📍 DODOMA

MAADHIMISHO ya miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yameambatana na wito wa kutunza miti iliyopandwa pamoja na kulinda miundombinu ya shule mpya ya Msingi Nanenane, ili kudumisha mazingira bora ya kujifunzia, kufundishia na kuenzi tunu za umoja na maendeleo.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Alhaj Jabir Mussa Shekimweri ambae ni mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alisisitiza kuwa utunzaji wa mazingira ya shule na miundombinu yake ni jukumu la pamoja kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Alieleza kuwa kupanda miti ni hatua muhimu katika kukijanisha mazingira. “Lakini niseme kuwa, ni lazima miti hii ifuatiliwe na utunzaji uwe endelevu ili miti hiyo iweze kukua na kutoa kivuli, hewa safi na kupendezesha mazingira ya shule” alisema Alhaj Shekimweri.

Aidha, alihimiza matumizi ya mbinu rahisi ya kumwagilia miti hiyo ili ikue vizuri na kuleta tija. “Kuna njia rahisi mnaweza kuitumia ambayo ni kutumia chupa za maji ambayo mtatoboa matundu madogo kwa ajili ya umwagiliaji wa taratibu, hasa katika kipindi cha ukame” alihimiza Alhaj Shekimweri.

Nae, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Aziza Mumba alipongeza maandalizi na kuwakumbusha wananchi kuendelea kuuenzi muungano kwakuwa unaleta tija katika nyanja zote zinazochochea maendeleo ya kiuchumi.

Katika maadhimisho hayo, jumla ya miti 250 ilipokelewa shuleni hapo ambapo miti 162 ilipandwa na miti 88 iliyobaki iligawiwa kwa wananchi ikiwa ni ujumbe wa kuuenzi muungano kwa vitendo, kwa kulinda mazingira, kutunza rasilimali zilizopo na kuimarisha mshikamano wa jamii.