Na Na John Bukuku, Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, amesema ZIARA YA KIHISTORIA YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA BELARUS YAIMARISHA USHIRIKIANO NA TANZANIA ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Belarus nchini Tanzania ni ya kihistoria, ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika baada ya miaka 30 ya mahusiano ya kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Wizara ya Mambo ya Nje jijini Dar es Salaam Aprili 28, 2026, Kombo alisema ziara hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya uhusiano ulioanzishwa mwezi Mei, na kwamba inalenga kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa karibu na wenye tija zaidi.
Alisema Tanzania inatarajia pia kupokea ziara ya Waziri Mkuu wa Belarus siku zijazo, kufuatia ziara ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, aliyefanya ziara nchini humo mwaka jana, hatua inayoashiria kuimarika kwa mahusiano ya pande mbili.
Kwa mujibu wa Kombo, pande hizo zimekubaliana kuimarisha mawasiliano ya kidiplomasia ambayo kwa muda mrefu hayakuwa ya karibu licha ya mahusiano kudumu kwa miongo mitatu, huku kipaumbele kikubwa kikiwekwa katika diplomasia ya uchumi.
“Tumekubaliana kwamba miaka miwili ijayo itakuwa na mafanikio makubwa kuliko miaka 30 iliyopita, kutokana na kasi ya utekelezaji wa makubaliano tuliyofikia,” alisema Kombo.
Aliongeza kuwa tayari mikataba mbalimbali ipo katika hatua za mwisho na mingine inatarajiwa kusainiwa, ikihusisha sekta za kilimo, elimu, afya, nishati na uwekezaji, kwa lengo la kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi wa nchi hizo mbili.
Katika sekta ya kilimo, alisema Tanzania itanufaika na teknolojia ya kisasa kutoka Belarus, huku ushirikiano huo ukijikita pia katika usalama wa chakula na mageuzi ya kilimo kupitia matumizi ya mitambo na utaalamu wa hali ya juu.
Alibainisha kuwa ushirikiano huo utajumuisha pia mafunzo kwa wanafunzi wa Tanzania katika fani mbalimbali, pamoja na kubadilishana wanafunzi kupitia vyuo vikuu vya Sokoine University of Agriculture, Mzumbe University na State University of Zanzibar pamoja na vyuo vya Belarus.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Belarus, Maxim Ryzhenkov, alisema nchi yake inaona Tanzania kama mshirika muhimu barani Afrika, na kwamba ipo tayari kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Alisema Belarus ina uwezo mkubwa katika teknolojia ya kilimo, uzalishaji wa viwandani na dawa, na kwamba wako tayari kushiriki kikamilifu katika programu za maendeleo ya kilimo nchini Tanzania ili kusaidia kukabiliana na changamoto za usalama wa chakula.
“Tumejadiliana miradi ya pamoja ikiwemo kuanzisha ubia katika tiba za mifugo kwa kutumia teknolojia ya Belarus, pamoja na usambazaji wa dawa bora, na tunaamini matokeo ya ushirikiano huu yatanufaisha moja kwa moja wananchi,” alisema Ryzhenkov.
Aliongeza kuwa Belarus inatarajia kuwapokea maafisa na wafanyabiashara wa Tanzania katika maonesho ya kimataifa ya kilimo mwaka 2026, sambamba na kuendeleza ushirikiano wa elimu kupitia kubadilishana wanafunzi, wataalamu na kushiriki katika tafiti na mikutano ya kisayansi.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mfumo wa kisheria wa ushirikiano wa pande mbili pamoja na kuunda kamati ya pamoja ya biashara na uchumi, hatua itakayosaidia kukuza zaidi mahusiano ya kiuchumi na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili.





