MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Hamza Johari akizungumza kwenye mkutano huo jijini Arusha leo
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, amesema kuwa ,ufanisi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali unategemea kwa kiasi kikubwa nidhamu, uadilifu na mshikamano wa watumishi wake, huku akisisitiza kuwa utoaji wa huduma bora za kisheria unapaswa kuendana na matarajio ya wadau wa Serikali na wananchi kwa ujumla.
Ameyasema hayo jijini Arusha wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Baraza la Wafanyakazi wa ofisi hiyo unaofanyika jijini Arusha .
Johari amesisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya muda wa kazi pamoja na uwajibikaji wa kila mtumishi katika nafasi yake.
Aidha Johari amewataka watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na weledi ili kuhakikisha taasisi hiyo inatimiza kikamilifu wajibu wake wa kikatiba na kisheria kwa manufaa ya Taifa.
“Tuna wajibu wa kuhakikisha tunatoa huduma za kisheria kwa ubora, ufanisi na tija inayotarajiwa. Hili linawezekana endapo kila mmoja atatekeleza majukumu yake kwa nidhamu na kujituma,” amesema Johari.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya kisheria ili kuhakikisha inakuwa imara na yenye kuongoza mwelekeo wa maendeleo ya Taifa.
“Sheria ni msingi wa maendeleo ya nchi. Bila mifumo imara ya kisheria, Taifa linaweza kupoteza dira yake,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Naibu Mwanasheria Mkuu wa serikali , Samweli Maneno, amesema ofisi hiyo imeendelea kupata mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yake kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya watumishi na menejimenti.
Ameongeza kuwa, hali hiyo imechangia kuimarika kwa utendaji kazi, hususan katika usimamizi wa mikataba ya Serikali na matumizi bora ya rasilimali za umma.
Maneno amefafanua kuwa pamoja na changamoto zilizopo, ofisi imeendelea kuboresha mazingira ya kazi, kuwekeza katika rasilimali watu na kutoa mafunzo yanayowawezesha watumishi kuendana na mabadiliko ya kitaaluma.
“Baraza la Wafanyakazi litaendelea kusimamia maslahi ya watumishi huku likihimiza uwajibikaji na kuongeza ufanisi wa taasisi hiyo.”amesema Maneno.
Katika hatua nyingine, mkutano huo ulienda sambamba na uchaguzi wa viongozi wa Baraza la Wafanyakazi, hatua inayolenga kuimarisha uwazi na ushirikishwaji wa watumishi katika maamuzi ya taasisi.
Awali, akiwasilisha Risala ya Wafanyakazi, Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Rashidi Kigalu ameushukuru na kuupongeza uongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuboresha mazingira na maslahi ya Watumishi, yanayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
“Kwa niaba ya Watumishi natoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu, Naibu Mwanasheria Mkuu na Menejimenti kwa ujumla kwa kuboresha maslahi na mazingira ya kazi kwa watumishi.” Amesema Kigalu .
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wamefanya uchaguzi kwa kuwachagua Bw. William Mudogo kuwa Katibu na Bi. Fay Grace Sadallah kuwa Katibu Msaidizi wakichukua nafasi hizo baada ya Bi. Beatrice Nzobonaliba na Hassan Nkya waliomaliza muda wao.





