Na Silivia Amandius
Bukoba.
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mhe. Erasto Sima, Aprili 27, 2026 amefungua kikao cha wadau wa zao la kahawa kilichofanyika katika Ukumbi wa Chemba, akihimiza ushirikiano na uwajibikaji ili kuinua uzalishaji wa zao hilo muhimu kiuchumi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mhe. Sima amesema Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba ina nafasi kubwa katika uzalishaji wa kahawa, hivyo kikao hicho kiwe jukwaa la wadau kubadilishana uzoefu kwa kuainisha mafanikio, changamoto na mikakati ya kuboresha sekta hiyo.
Alisisitiza kuwa kila mdau anatakiwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo ili kufikia matokeo chanya, akibainisha kuwa uwajibikaji wa pamoja ndiyo msingi wa mafanikio endelevu katika kilimo cha kahawa.
Aidha, Mhe. Sima alieleza kuwa ubora wa kahawa una mchango mkubwa katika bei ya soko, hivyo ni muhimu kwa wakulima kupatiwa miche bora na elimu ya kisasa ya kilimo, pamoja na kudhibiti vitendo vya magendo na uvunaji wa kahawa mbichi ili kulinda ubora wa zao hilo.
Katika kikao hicho, wadau walijadili hali ya uzalishaji wa kahawa inayokadiriwa kufikia wastani wa kilo 700 hadi 1200 kwa hekta, pamoja na mikakati ya kuongeza uzalishaji ikiwemo upanuzi wa maeneo ya kilimo na usambazaji wa miche bora. Hata hivyo, changamoto kama magonjwa, wadudu waharibifu, mnyauko, kupungua kwa rutuba ya udongo, ukosefu wa mitaji na mabadiliko ya tabia ya nchi ziliendelea kujitokeza.





