Na Hellen Mtereko,Mwanza
Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mabatini, mkoani Mwanza, Mrakibu wa Polisi (SP) Daktari Steven Kisaka, amewashauri wakazi wanaoishi karibu na zahanati hiyo iliyopo wilayani Nyamagana, kuitumia kikamilifu kwa ajili ya kupata matibabu pindi wanapougua.
Daktari Kisaka ametoa ushauri huo Aprili 26, 2026, wakati akishiriki kufanya usafi wa mazingira ya zahanati hiyo na wadau wa maendeleo kutoka kikundi cha “Upendo Federation” cha Kata ya Mabatini, kinachojihusisha na huduma mbalimbali za kijamii.
Daktari Kisaka, ambaye pia ni Mkuu wa Zahanati hiyo, amesema wataendelea kutoa huduma bora za afya na za uhakika kwa wagonjwa watakaofika kupata matibabu, wakizingatia weledi wa Jeshi la Polisi.
Mwenyekiti wa kikundi cha Upendo Federation, Seleman Kapera, amesema kuwa wamefika katika zahanati hiyo kufanya usafi kwa kutambua kuwa usafi ni afya, na wataendelea na utaratibu huo katika maeneo mbalimbali.
Kwa upande wake, Polisi Kata ya Mabatini, Mkaguzi wa Polisi (Insp) Shabani Kashakala, amesema tangu kianzishwe, kikundi hicho kimekuwa kikishiriki katika shughuli za usafi wa mazingira na kusaidia kudhibiti uhalifu.
Kashakala amesema kupitia kikundi hicho, wamekuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kutunza amani na kuwa wazalendo, hususan kwa vijana ambao wamekuwa mstari wa mbele kujiingiza katika makundi hatarishi.
Zoezi hilo liliambatana na utoaji wa msaada wa sabuni kwa wagonjwa waliolazwa katika zahanati hiyo. Wagonjwa hao wamesema huduma wanayopata kutoka kwa madaktari ni nzuri na wanaendelea vyema, huku wakiwashukuru wadau hao kwa msaada wao.
Ujio wa kikundi hicho cha kijamii cha Upendo Federation katika zahanati hiyo kufanya usafi ni ishara tosha kuwa dhana ya Polisi Jamii inatekelezwa kwa vitendo.
Zahanati ya Polisi Mabatini hupokea wagonjwa kati ya 60 hadi 100 kwa siku wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali, huku kina mama wawili hadi watatu wakijifungulia katika zahanati hiyo kila siku.
Muonekano wa Zahanati ya Mabatini iliyoko Jijini Mwanza





