Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imepokea vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa kimaabara kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia Dawa za Kulevya na Uhalifu, ikiwa ni ishara ya pongezi kufuatia mafanikio yaliyofikiwa na Tanzania katika kudhibiti dawa za kulevya nchini.
Pongezi hizo zimetolewa Aprili 22, 2026 jijini Dar es Salaam na ujumbe wa UNODC ulioongozwa na Mwakilishi wa Kanda ya Afrika Mashariki, Ali El-Bereir, ambaye ameipongeza Tanzania kwa jitihada zake katika kudhibiti biashara na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kemikali bashirifu.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, El-Bereir amesema kuwa mafanikio ya Tanzania ni kielelezo cha dhamira thabiti ya Serikali na taasisi zake katika kuhakikisha jamii inalindwa dhidi ya athari za dawa za kulevya. Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na UNODC utaendelea kuimarishwa ili kudhibiti mtandao wa biashara hiyo haramu.
Vifaa hivyo vimetolewa mahsusi kuzijengea uwezo taasisi zinazohusika na udhibiti wa dawa za kulevya katika ngazi ya kimataifa, chini ya mpango wa Port Security and Safety of Navigation Programme (EU PSP), unaolenga kuimarisha usalama wa bandari na usafirishaji wa kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, vifaa hivyo ni pamoja na mashine za kisasa zenye uwezo wa kubaini kwa haraka aina mbalimbali za dawa za kulevya na kemikali zinazodhibitiwa, hata zikiwa ndani ya vifungashio vyake bila kufunguliwa. Teknolojia hiyo inatarajiwa kuongeza ufanisi wa uchunguzi na kuboresha utendaji kazi wa DCEA.
Aidha, UNODC imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa kutoa mafunzo na kuwajengea uwezo maafisa wa DCEA, hatua itakayosaidia kuimarisha zaidi mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini.
Kupokelewa kwa vifaa hivyo kunatajwa kuwa ni hatua muhimu katika juhudi za Serikali za kuhakikisha udhibiti madhubuti wa dawa za kulevya na kulinda afya pamoja na ustawi wa jamii.





