Na Silivia Amandius.
Bukoba
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kagera, Ndg. Faris Buruhan, ametoa wito kwa vijana kuzingatia umoja, ushirikiano na kulinda amani ya nchi, wakati akizindua rasmi mashindano ya vijana ya mpira wa miguu katika manispaa ya bukoba.
Akizungumza katika uzinduzi wa UVCCM CUP Leo April 24, mwaka huu Buruhan amesisitiza kuwa vijana wana nafasi kubwa katika kujenga jamii yenye mshikamano na maendeleo, akibainisha kuwa michezo ni moja ya njia muhimu ya kuwaunganisha vijana na kuwaepusha na vitendo visivyofaa.
Alieleza kuwa mashindano hayo, yanayoshirikisha timu 14 kutoka kata mbalimbali za Bukoba Mjini, yanapaswa kuwa jukwaa la kuwakutanisha vijana wote bila kujali tofauti za kisiasa, ili kujenga urafiki, kuheshimiana na kuimarisha amani.
“Mashindano haya yawakusanye vijana wote, yawe chachu ya umoja na mshikamano, lakini pia yawajenge vijana kuwa walinzi wa amani ya nchi yetu, pia yasiwe mashindano ya kubaguana au ya vijana wa CCM Bali ni ya vijana wote” alisema Buruhan.
Aidha, alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba Mjini, Ndugu James Nyamanza, kwa kuanzisha mashindano hayo yenye lengo la kukuza vipaji na kuimarisha mahusiano chanya miongoni mwa vijana.
Kwa upande wake, Nyamanza alisema kuwa mashindano hayo yameandaliwa ili kuwapa vijana nafasi ya kuonyesha vipaji vyao na kujenga mtandao wa mahusiano utakaosaidia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji, kuimarisha maadili na kukuza mshikamano wa vijana kati manispaa ya Bukoba.





