Katikati ni Naibu waziri wa uchukuzi David Kihenzile katika uzinduzi wa kiwanja cha ndege cha Sumbawanga
Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika uzinduzi wa kiwanja cha ndege cha Sumbawanga
Viongozi mbalimbali walioshiriki katika uzinduzi wa kiwanja cha ndege cha Sumbawanga
Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini Aesh Hilary wakati akizungumza katika uzinduzi huo
Wabunge wa mkoa wa Rukwa wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu waziri Kihenzile.
………………
Na Neema Mtuka – Sumbawanga
David Kihenzile amewataka wananchi kutumia vyema fursa zilizopo ili kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha miradi ya kimkakati, akisisitiza kuwa sekta ya uchukuzi ni mhimili muhimu wa maendeleo kwa kuwa imeboresha huduma za usafiri na usafirishaji nchini.
Kihenzile amesema hayo Aprili 24, 2026 wakati akimwakilisha Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa, katika uzinduzi wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga mkoani Rukwa.
Amesema uwanja huo ni kichocheo muhimu cha maendeleo kwa wananchi wa mkoa huo pamoja na maeneo jirani, na kwamba utarahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii.
Aidha, amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali itaendelea kuboresha sekta ya uchukuzi ili kuinua maisha ya wananchi kwa ujumla.
Katika uzinduzi huo, ndege ya abiria ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) aina ya Dash 8 Q400 imetua kwa mara ya kwanza katika uwanja huo na kupokelewa kwa heshima ya “water salute”, kuashiria kuanza rasmi kwa huduma za usafiri wa anga katika eneo hilo.
“Ninazindua uwanja huu wa ndege kwa kuwa umejengwa kwa kiwango kinachokubalika, ukiwa na ubora wa hali ya juu wa kimataifa,” amesema Kihenzile.
Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Msalika Makungu, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Charles Makongoro Nyerere, amesema uzinduzi wa uwanja huo utafungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wakazi wa mkoa huo.
Baadhi ya wananchi, akiwemo Mikidadi Machesha, ambaye alikuwa msafiri wa kwanza baada ya uzinduzi huo akitokea Sumbawanga kuelekea Dar es Salaam, amesema huduma hiyo imerahisisha safari na kupanua wigo wa ajira.
“Kiwanja hiki kitachochea maendeleo makubwa kwa mkoa wa Rukwa. Zamani tulikuwa tunasafiri umbali wa kilomita 1,148 kuelekea Dar es Salaam, lakini sasa ni saa moja na dakika 40 tu,” amesema Machesha.
Ameiomba mamlaka ya uwanja huo kuhakikisha kunakuwa na safari za kila siku, akieleza kuwa uwanja huo ni lango muhimu la usafiri kwa mikoa na nchi jirani kama Zambia na Congo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Abdul Mwondokaleo, amesema uwanja huo una uwezo wa kuhudumia hadi abiria 150,000 kwa mwaka, huku akibainisha kuwa kwa sasa abiria watanufaika na nauli nafuu zilizopunguzwa.
Ujenzi wa uwanja huo umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 60 hadi kukamilika kwake.
Naye Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini, Aesh Halfani Hilary, amewahimiza wananchi kuchangamkia fursa zilizopo ikiwemo ajira, biashara na utalii ili kuongeza kipato cha mkoa na taifa kwa ujumla.
Aidha, amemwomba Naibu Waziri wa Uchukuzi kuharakisha ukarabati wa meli ya MV Liemba katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, ili kuongeza fursa za usafiri na biashara kwa wakazi wa Rukwa.
“Nimeupigania uwanja huu kwa zaidi ya miaka kumi, hivyo uzinduzi wake utarahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wakazi wa Sumbawanga,” amesema Aesh.




