*Lengo ni kuongeza tija kwa wachimbaji wadogo
*Yashauriwa kufufua mpango wa Benki ya Madini
*FEMATA kufaidika na Utafiti wa kina
Dodoma
Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) limeshauriwa kuanza kufanya utafiti wa masoko ya madini ndani na nje ya nchi ili kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata tija zaidi kutokana na rasilimali madini zilizopo nchini.
Ushauri huo umetolewa leo Aprili 24, 2026 na Waziri wa Madini Anthony Mavunde katika mkutano maalum uliohusisha shirikisho la FEMATA na Wataalamu wa Wizara ya Madini ukiwa na lengo la kujadili mkakati wa uchumi wa kufikia dola trilioni moja.
Waziri Mavunde ameongeza kwamba kuwepo kwa utafiti huo utasadia wachimbaji wadogo kufahamu mnyororo wa thamani na bei elekezi za kimataifa, jambo litakalo punguza utegemezi kwa madalali wanaonunua madini kwa bei ya chini.
Waziri Mavunde amefafanua kuwa, kwasasa Serikali inakuja na mpango kamili utakaoanzia utafiti awali utakaofanywa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ambao utaendeleza utafiti wa kina wa STAMICO kwa lengo la kuvumbua maeneo mapya ya rasilimali madini.
Aidha, Mavunde ameitaka FEMATA kuongeza mashirikiano na taasisi za Wizara ya Madini katika kukusanya takwimu ili kuongeza ufahamu kwa wanachama wake hususan katika taarifa za mwenendo wa sekta ya madini kwenye utafiti, uchimbaji , uchenjuaji na masoko.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa amemuelekeza Katibu Mtendaji Tume ya Madini kuandaa utaratibu mzuri wa kugawa leseni zilizofutwa kwa wachimbaji wadogo kwenye maeneo yao ili kuongeza tija ya uzalishaji madini kila mkoa.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt.Venance Mwase ameishauri FEMATA kuendelea na mpango wake wa kufungua Benki ya madini ili kupunguza changamoto za kiuchumi zinazowakabili wachimbaji wadogo katika shughuli zao.
Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wadogo nchini, Rais wa FEMATA John Bina ameishukuru Wizara ya Madini kwa ushauri na ushirikiano mzuri inayotoa kwa wachimbaji wadogo kuanzia vifaa , mashine za uchorongaji miamba na kuwaunganisha na taasisi za kifedha jambo linaloleta mageuzi makubwa kwa wachimbaji wadogo nchini.





