Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Constantine Sima, ambaye ndiye Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa nchini (ALAT) akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Njombe Agnetha Mpangile ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Alat Taifa akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha .
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Constantine Sima, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa nchini (ALAT) baada ya kuibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi uliofanyika leo jijini Arusha.
Aidha katika mkutano huo pia ,Mwenyekiti wa halmashauri ya Njombe Agnetha Mpangile amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Alat Taifa katika uchaguzi huo.
Katika uchaguzi huo uliovutia ushindani mkali, Sima alipata kura 273 kati ya kura halali 338, akimuacha mbali mpinzani wake wa karibu, Meya wa Jiji la Arusha, Maxmillian Ilange, aliyepata kura 45.
Ushindi huo mkubwa unaakisi imani na matarajio makubwa ya viongozi wa serikali za mitaa kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa Sima, ambaye sasa anakabidhiwa jukumu zito la kuongoza na kuratibu shughuli za ALAT katika kipindi kijacho.
Sima amesema kuwa , anatarajiwa kusukuma mbele ajenda za msingi za mamlaka za serikali za mitaa, ikiwemo kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi, kuongeza uwajibikaji, pamoja na kutetea maslahi ya halmashauri mbele ya Serikali Kuu na wadau wa maendeleo.
Jumuiya ya Tawala za Mitaa nchini (ALAT) ni chombo muhimu kinachowakutanisha viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa, kikilenga kuimarisha ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kusukuma mbele agenda za maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika ngazi ya halmashauri.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti huyo, Mpangile ameshukuru wajumbe hao kwa kumchagua huku akiaahidi kuwawakilisha vyema katika nafasi yake hiyo na kuomba ushirikiano wa karibu katika kufanikisha malengo hayo.
Aidha Mpangile ameshinda nafasi hiyo baada ya kuchaguliwa na wajumbe wa mkutano huo ambapo amewashukuru wajumbe hao kwa kumwamini na kumpa nafasi hiyo .
“Nashukuru sana kwa kuniamini na kunionyesha imani na mimi.nitawaonyesha imani mliyonipa na nitaendelea kuwahitaji katika ushauri mbalimbali katika kuujenga umoja wetu”amesema Mpangile .





