Serikali Kupitia ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI imeeleza kuwa ipo katika hatua za kuanza ujenzi wa soko la kisasa la mnada wa mifugo katika Wilaya ya Meatu, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya biashara ya mifugo na kuongeza mapato ya Halmashauri.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni leo Aprili 24, 2026 na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Mhe. Dkt. Festo Dugange, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Meatu, Mhe. Salum Khamis Salum, kuhusu lini Serikali itaanza ujenzi wa Soko la Mnada wa Mifugo ili kuwa na Soko lenye hadhi na kuongeza mapato ya Halmashauri katika Jimbo la Meatu
Akijibu swali hilo, Mhe. Dkt. Dugange anasema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu tayari ina minada minne ya awali ambayo ni Bukundi, Itinje, Mwanhuzi na Tindabuligi, lakini inahitaji kuboreshwa ili kukidhi mahitaji ya sasa ya soko la mifugo. Amesisitiza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha miundombinu hiyo ili kuweka mazingira rafiki kwa wafugaji na wanunuzi.
Amefafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2023/24, halmashauri ilitumia shilingi milioni 14.3 kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya maboresho ya awali, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa machinjio, vyoo na kutenga eneo la ekari nane kwa ajili ya mnada wa kisasa katika kijiji cha Bukundi. Hatua hiyo inaonekana kuwa msingi muhimu kuelekea utekelezaji wa mradi mkubwa zaidi wa soko hilo.
Aidha, Mhe. Dkt. Dugange amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26, Halmashauri imetenga shilingi milioni 12 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa awamu ya kwanza wa uzio wa mnada huo. Amesema ujenzi huo unatarajiwa kuanza mwezi Mei 2026 huku taratibu nyingine za upatikanaji wa fedha za ujenzi wa soko zikiendelea kukamilishwa.
Katika hatua nyingine, Serikali imeahidi kushughulikia changamoto ya ukosefu wa mizani katika minada hiyo, ambapo Mhe. Dkt. Dugange amesema kuwa kwa kushirikiana na wizara husika, watahakikisha mizani inapatikana ili kuwezesha uuzaji wa mifugo kwa kuzingatia uzito badala ya makadirio, hatua itakayoongeza uwazi na tija katika biashara hiyo.





