Na. John Bukuku- Dar es salaam
Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29, 2025, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande amesema uchambuzi wa kisheria na ushahidi uliokusanywa unaonyesha kuwa matukio yaliyotokea siku hiyo hayakuwa maandamano ya amani, bali ghasia zilizoambatana na uvunjifu wa amani.
Akiwasilisha ripoti ya Tume hiyo Aprili 23, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Jaji Chande amesema uamuzi huo umetokana na tathmini ya sheria za nchi, ikiwemo taratibu za kutoa notisi kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya maandamano, ambazo hazikuzingatiwa.
Kwa mujibu wa Tume, siku ya Oktoba 29, 2025 ilitangazwa kisheria kuwa ni siku ya uchaguzi mkuu, hivyo matukio yaliyotokea yalivuruga haki ya wananchi kushiriki uchaguzi huo kama ilivyokusudiwa kikatiba.
Aidha, Jaji Chande amesema washiriki wa vurugu hizo walitumia silaha mbalimbali zisizoruhusiwa kisheria katika maandamano ya amani, zikiwemo mawe, nondo, mikuki, visu, mapanga, fimbo na silaha nyingine za kujihami na kushambulia, hali iliyochochea taharuki na uharibifu wa mali pamoja na kuhatarisha maisha ya watu.
Tume pia imebainisha kuwa sheria na taratibu za kitaifa, kikanda na kimataifa haziruhusu maandamano
yanayosababisha hofu kwa wananchi, kuvuruga usalama wa taifa au kuhatarisha maisha ya watu wengine.
Katika uchunguzi wake wa kidijitali, Tume hiyo imegundua uwepo wa picha na video zilizosambaa mitandaoni wakati wa tukio hilo, ambazo zilithibitishwa kuwa si halisi, bali zilihaririwa kwa kutumia teknolojia ya akiliunde (AI) ili kuaminisha umma kuwa kulikuwa na vifo na maafa makubwa.
Jaji Chande ametoa mfano wa picha iliyokuwa ikionesha miili ikiwa kwenye mifuko ya plastiki na inadaiwa kuzikwa kwenye makaburi ya pamoja, akisema picha hiyo imetumika mara kwa mara katika maeneo mbalimbali duniani na si tukio la Tanzania.
Tume hiyo imeeleza kuwa ilikusanya jumla ya vielelezo vya kidijitali vikiwemo picha mnato 450 na video 880 kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, vyombo vya habari, mashuhuda pamoja na taasisi za ulinzi na usalama.
Kwa mujibu wa Jaji Chande, uchambuzi huo ulifanywa kwa kutumia mbinu za kitaalamu za uthibitishaji ili kuhakikisha taarifa zote zinakidhi viwango vya kimataifa vya uchunguzi na ukweli wa ushahidi.





