Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Pili ya Wadhamini ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Aprili 23, 2026 jijini Dodoma.
Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema kuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa ni kioo cha Dodoma na taifa kwa ujumla, akieleza kuwa ubora wa huduma zinazotolewa umeifanya hospitali hiyo kutozungumzwa kwa malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi kama ilivyo katika baadhi ya maeneo ya sekta ya afya.
Amesema kuwa hospitali hiyo iliyopo makao makuu ya nchi imeendelea kuonesha mfano mzuri wa utoaji huduma, akiwapongeza viongozi wa bodi na menejimenti kwa kazi wanayoifanya kwa ufanisi mkubwa.
ameyabainisha hayo Aprili 23,2026, Jijini Dodoma alipokuwa akizindua Bodi ya pili ya Wadhamini ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH).
Aidha, amebainisha kuwa Mwenyekiti wa Bodi ameonesha uongozi mzuri hata katika mazingira magumu, huku akimpongeza pia Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo kwa mafanikio yanayoonekana wazi katika uendeshaji wa taasisi hiyo.
Pia ameongeza kuwa mazingira ya hospitali hiyo ni safi na yenye kuvutia kiasi cha kumfanya mtu ajisikie kama yupo hotelini badala ya hospitali, hali inayoashiria dhamira ya dhati ya kuifanya kuwa hospitali ya taifa.
Mchengerwa amesema kuwa serikali inalenga kuifanya Hospitali ya Benjamin Mkapa kuwa hospitali ya taifa ili iweze kutoa huduma zote muhimu katika sekta ya afya, sambamba na kuimarisha utalii wa tiba nchini.
Aidha amebainisha kuwa haiwezekani maamuzi makubwa ya sekta ya afya yaendelee kufanyika nje ya makao makuu ya nchi, akisisitiza kuwa Dodoma inapaswa kuwa kitovu cha maamuzi hayo.
Pia ameongeza kuwa wizara ipo tayari kushirikiana na bodi hiyo mpya kuhakikisha mageuzi katika sekta ya afya yanafanikiwa, huku akisisitiza umuhimu wa viongozi na watumishi kufanya kazi kwa kujitolea muda wote kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Awali akizungumza, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Edward Hoseah, amesema kuwa jukumu kuu la bodi hiyo ni kusimamia na kuishauri taasisi ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, ikiwemo kutoa huduma za kibingwa na bobezi, mafunzo pamoja na kufanya tafiti.
Aidha amebainisha kuwa bodi hiyo mpya ipo tayari kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa kuhakikisha hospitali inaendelea kutoa huduma katika viwango bora na vya kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi, amesema kuwa hospitali hiyo imepiga hatua kubwa katika huduma za kibingwa ikiwemo upandikizaji wa figo, upasuaji wa moyo, ubongo na huduma za mfumo wa mkojo.
Pia ameongeza kuwa kwa sasa hospitali hiyo ina huduma za kibingwa 20 na huduma za kibingwa bobezi 17, akieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi za serikali pamoja na mchango wa Rais Samia Suluhu Hassan.




