Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Riziki Shemdoe akizungumza kwenye mkutano huo jijini Arusha.

Mkurugenzi Mtendaji wa TAASISI ya (TARSI) ,Maliki Barongo akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha

Meneja wa Usalama na Usanifu wa Barabara , Injinia Laurent Maganga akizungumza na waandishi wa habari.

Mwenyekiti wa Bodi ya TARSI, Vincent Minja akifafanua jambo kuhusi mkutano huo jijini Arusha
…………..
Na Happy Lazaro ,Arusha .
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Riziki Shemdoe amesema kuwa Taasisi ya TARSI imekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya uhandisi nchini tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002, ambapo tayari imeshatoa mafunzo kwa wahandisi zaidi ya 800.
Waziri Shemdoe ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya kitaalamu ya wadau wa usalama barabarani yaliyofanyika jijini Arusha.
Waziri Shemdoe amesema mafunzo hayo ni chachu muhimu katika jitihada za kupunguza ajali za barabarani nchini ambapo amesema akisisitiza kuwa ni lazima mafunzo hayo yaendelee kuimarishwa na kupanuliwa ili kuongeza ufanisi wa wataalamu wa uhandisi.
Aidha, ameitaka TARURA kuhakikisha inaandaa na kuratibu mafunzo ya mara kwa mara kwa wahandisi wake, ili kuwezesha ujenzi na ukarabati wa barabara unaozingatia viwango na alama za kimataifa, hatua ambayo itaongeza ubora wa miundombinu na kupunguza hatari za ajali barabarani.
Mkurugenzi Mtendaji wa TAASISI ya Mpango wa Usalama Barabarani Tanzania (TARSI) ,Maliki Barongo, amesema mapambano dhidi ya ajali hayawezi kufanikiwa bila elimu kuanzia ngazi ya usanifu hadi kwa watumiaji wa mwisho wa barabara.
Barongo amesema kuwa ,
TARSI imesema itaendelea kuongoza juhudi za kupunguza ajali za barabarani nchini kwa kuwekeza zaidi katika elimu ya usalama, uboreshaji wa usanifu wa miundombinu na ushirikiano wa karibu kati ya wadau wote wa sekta ya usafiri.
Barongo amesema elimu ya usalama barabarani ndiyo silaha ya msingi katika kupunguza vifo vinavyotokana na ajali, akisisitiza kuwa changamoto nyingi huanzia kwenye hatua za awali za ujenzi wa barabara.
“Usalama barabarani hauanzi barabarani, unaanzia kwenye meza ya usanifu. Kama wahandisi watazingatia viwango vya usalama, tunapunguza kwa kiasi kikubwa hatari zote zinazoweza kuzuilika,” amesema Barongo.
Amebainisha kuwa hadi sasa TARSI imewafikia zaidi ya wahandisi 800 waliopatiwa mafunzo maalum ya kuzingatia usalama katika miradi ya barabara, hatua inayolenga kuhakikisha miundombinu inakuwa rafiki kwa watumiaji wote.
“Taasisi hiyo pia imeweka programu za kuwafikia madereva kwa kushirikiana na kampuni za usafirishaji pamoja na kampeni za elimu kwa watembea kwa miguu, ili kujenga tabia salama katika matumizi ya barabara.”amesema Barongo.
Mwenyekiti wa Bodi ya TARSI, Vincent Minja, amesema suluhisho la ajali linahitaji ushirikiano wa serikali, sekta binafsi na jamii, kuanzia hatua ya kupanga na kubuni barabara.
Amefafanua kuwa , miundombinu mingi bado haizingatii usalama wa watembea kwa miguu, waendesha baiskeli na bodaboda, hali inayochangia ongezeko la ajali.
“Tunahitaji kuhakikisha kila barabara inazingatia usalama tangu hatua ya usanifu,” amesema.
Alibainisha pia kuwa taasisi kama TANROADS, TARURA na Road Fund Board (Tanzania) zimehusishwa ili kupata suluhisho la pamoja.
Meneja wa Usalama na Usanifu wa Barabara , Injinia Laurent Maganga, amesema elimu ya usalama barabarani inapaswa kuingizwa rasmi kwenye mitaala ya uhandisi ili kuhakikisha wataalamu wanajenga miundombinu salama na yenye kuzingatia maisha ya watu.
“Ajali zinaendelea kuigharimu nchi kwa kupoteza maisha, ulemavu na gharama kubwa za matibabu, hali inayohitaji hatua za haraka.”amesema Maganga.




