Na Mwandishi Wetu, Tabora
SIKONGE, TABORA: Mashamba darasa ya kilimo na malisho ya mifugo yameibuka kuwa suluhisho la kuongeza uzalishaji na kupunguza uharibifu wa misitu wilayani Sikonge, mkoani Tabora, kupitia Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo.
Mbinu zinazotumika katika mashamba hayo, ikiwemo matumizi ya mbegu bora, upandaji kwa wakati na kilimo cha kuongeza rutuba ya udongo, zinaongeza tija kwa wakulima na wafugaji huku zikilenga kupunguza utegemezi wa upanuzi wa mashamba katika maeneo ya misitu. Mbinu hizi zinatarajia kupunguza uharibifu wa misitu kwa kiasi kikubwa.
Aprili 21, 2026, wataalamu kutoka mashirika ya kijamii yanayoshirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) walitembelea mashamba hayo kujifunza na kubadilishana uzoefu. Ziara hiyo ilihusisha pia wataalamu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wakiongozwa na Mratibu wa Mradi, Dkt. Zainabu Bungwa.
Mashamba darasa yaliyopo kijiji cha Ipole, yanayomilikiwa na vikundi vya Uwani, Ulelema na Kiwanu, yamekuwa mfano wa kuigwa kutokana na usimamizi bora na matokeo chanya ya uzalishaji wa mazao na malisho ya mifugo.
Katika ziara hiyo, wageni walikagua mashamba ya mahindi, karanga na maharagwe pamoja na shamba la mbegu za mihogo linalosimamiwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), na mashamba ya malisho chini ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI).
Akizungumza, mtafiti wa TARI, Dkt. Caroline Sichale, alisema mashamba darasa ni njia muhimu ya kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji na kipato kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa za kilimo.
Alieleza kuwa matumizi ya mimea inayoongeza rutuba ardhini kama gliricidia, maharagwe na mbaazi yanasaidia kuboresha udongo na kuongeza uzalishaji wa chakula.
Kwa upande wa mifugo, Afisa Mifugo wa Kata ya Ipole, Saitoti Koika, alisema elimu kwa wafugaji inaendelea kutolewa ili kuongeza tija na kuwafikia wafugaji wengi zaidi.
Mtaalamu kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Mazingira na Maendeleo (IIED), Stephen Mwangi, alisisitiza umuhimu wa wakulima na wafugaji kujiunga katika vikundi ili kuimarisha mnyororo wa thamani wa uzalishaji na biashara ya malisho.
Naye Isaack Bwire kutoka Taasisi ya IIRR ya Uganda alisema mafanikio ya mradi huo yanaweza kuwa mfano kwa nchi nyingine kutokana na mchango wake katika kuboresha maisha ya jamii.
Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo unatekelezwa katika mikoa ya Tabora na Katavi, ukihusisha wilaya za Sikonge, Urambo, Kaliua na Mlele, ukiwa na lengo la kuunganisha uhifadhi wa misitu na maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.





