Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani,Dkt.Vaneshwari Ashok Bamania akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kambi hiyo jijini Arusha .
……..
Na Happy Lazaro, Arusha
TANLINK Medical Tourism Agency kwa kushirikiana na Hospitali ya AGAKHAN iliyopo jijini Arusha na Mwanza na The Heart Medical Group kutoka California nchini Marekani wameandaa kambi ya matibabu ya kibingwa kwa magonjwa ya Moyo ,Ubongo na Mgongo chini ya madaktari kutoka Marekani na Tanzania (AgaKhan)
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani,Dkt.Vaneshwari Ashok Bamania amesema kuwa,kambi hiyo inaanza rasmi april 27 hadi mei 1 katika Hospitali ya AgaKhan Arusha.
Dkt.Bamania amesema kuwa,wananchi wote wanakaribishwa na kwa wale wote ambao wangependa kushiriki katika kambi hiyo wanatakiwa kujisajili kabla ya tarehe husika ya kambi kuanza kwa kufika katika Hospitali ya AgaKhan Arusha na Mwanza au katika ofisi za Tanlink Medical Tourism Agency zilizopo jijini Dar es Saalam wilaya ya Ilala .
“Kwa jiji la Mwanza kambi hiyo inatarajiwa kuanza mei 3 hadi mei 8,2026 katika hospitali ya Agakhan Mwanza hivyo nawaomba wananchi mbalimbali wajitokeze kwa wingi kushiriki kambi hiyo kwani ni fursa kwao kuweza kupata huduma ya matibabu hayo karibu .”amesema .
Ameongeza kuwa,kwenye kambi hiyo kutakuwa na Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kutoka California -Marekani Dkt.Munaf Shamji na Daktari Mugisha ambaye ni Daktari bingwa wa magonjwa ya kichwa ,Ubongo,mgongo na mishipa ya fahamu .
Aidha amesema kuwa,kambi hiyo ya matibabu ya kibingwa na bingwa bobezi ni muhimu sana kwa afya na jamii kwa ujumla kwa sababu ya ongezeko kubwa la magonjwa ya moyo uti wa mgongo na mgongo nchini Tanzania .
“Magonjwa haya ya moyo na mishipa ya damu yanachangia kwa sehemu kubwa ya vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza na kulingana na takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa takribani vifo 56,000 hutokea kila mwaka nchini Tanzania husababishwa na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.”amesema
Amefafanua kuwa,magonjwa haya mara nyingi huitwa muuaji wa kimya kimya kwa sababu watu wengi huwa nayo bila ya dalili zozote,na idadi kubwa ya wagonjwa bado hawajagundulika .
Dkt.Bamania ameongeza kuwa ,inakadiriwa kuwa asilimia 25 hadi 40 ya watu wazima nchini Tanzania wana shinikizo la damu,lakini wengi wao hawajui hali hiyo .
“Shinikizo la damu lisipogundulika mapema linaweza kusababisha madhara makubwa kama kiharusi shambulio la moyo,moyo kushindwa kufanya kazi ,figo kuharibika na hata kusababisha kifo cha ghafla “amesema Dkt.Bamania.
Ameongeza kuwa kupitia kambi hiyo ya afya wananchi watapata huduma za uchunguzi wa kitaalamu pamoja na vipimo muhimu kama ECG,ECHO na uchunguzi wa jumla wa afya .
“Tunapenda kuwahimiza wananchi wote wenye dalili kama maumivu ya kifua ,kupumua kwa shida,mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida,maumivu ya muda mrefu ya mgongo au shingo,ganzi au udhaifu wa viungo.
Napenda kutoa wito kwa kwa wananchi mbalimbali kutoka mkoa wa Arusha na nje ya hap kujitokeza kwa wingi kupima afya zao kwani lengo ni kutambua magonjwa mapema ,kutoa matibabu kwa wakati kuwasaidia wagonjwa kuelewa mwenendo wa ugonjwa wao na kupata ufuatiliaji sahihi na kuhakikisha mwendelezo wa huduma kwa wagonjwa wote.



