Na. Gladys Lukindo-BMH
MANYARA – APRIL 21, 2026
Kambi ya Uchunguzi na Matibabu inayoendeshwa na Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa kushirikiana na Madaktari wa Hospitali wa Mkoa wa Manyara imeanza rasmi katika Hospitali ya Mkoa wa Manyara na muitikio wa Wananchi ukiwa wa kuridhisha.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo na Huduma Mkoba wa BMH ambaye ndio kiongozi wa msafara Bi. Lilian Marwa amesema kuwa timu ya Madaktari Bingwa Bobezi kutoka BMH wamefika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, ambapo huduma zitakazo tolewa ni pamoja na matibabu ya Moyo , magonjwa ya ndani, mfumo wa mkojo, meno, mifupa, upasuaji wa Ubongo na mishipa ya fahamu.
“Tumekuja na madaktari bingwa hapa Hospitali ya mkoa wa Manyara kuanzia tarehe 20 hadi Ijumaa April 24, 2026 tukitoa huduma ya uchunguzi na matibabu kwa Wananchi, tunashkuru mwitikio wao umekuwa mzuri na wananchi wamejitokeza kwa wingi kupata huduma, ” amesema Bi. Lilian.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Manyara, Dkt. Yesige Mutajwa amewashukuru madaktari bingwa kwa ujio wao kwani wananchi watapata huduma nyingi. Akisema kuwa
“Tunashukuru kwa ujio wa madaktari bingwa waliokuja na magari yenye teknolojia kubwa Maalumu ambayo yana vyumba vya Upasuaji na vifaa tiba vingine vya kutolea huduma kupitia ujio huu tutaweza kuhudumia wananchi wengi zaidi kwa muda mfupi,” amesema Dkt. Mutajwa.
Hospitali ya Benjamin Mkapa imetoa madaktari na wataalamu kuhudumia wananchi, katika kuelekea hitimisho la kuadhimisha miaka kumi ya utoaji huduma zake tangia ilipo anzishwa.




