Waziri wa Fedha, Mhe. Khamis Mussa Omar (Mb)(kushoto), na Rais wa Benki ya Uwekezaji wa Miundombinu ya Asia (AIIB), Bi. Zou Jiayi, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukutana na kufanya mazungumzo, pembezoni mwa Mikutano ya Majira ya Kipupwe (Spring Meetings) ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, jijini Washington D.C, nchini Marekani, ambapo wamejadili kufungua fursa mpya za ufadhili kwa miradi ya kimkakati ya maendeleo, ikiwemo maji, nishati, usafiri, teknolojia ya habari na Mawasiliano pamoja na miundombinu ya kijani.
Na Benny Mwaipaja, Washington D.C
Tanzania imeendelea kuimarisha ushirikiano wake na Benki ya Uwekezaji wa Miundombinu ya Asia (AIIB), hatua inayotarajiwa kufungua fursa mpya za ufadhili kwa miradi ya kimkakati ya maendeleo, ikiwemo maji, nishati, usafiri, teknolojia ya habari na Mawasiliano pamoja na miundombinu ya kijani.
Hayo yamejiri wakati Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), alipo ongoza ujumbe wa Tanzania katika kikao na Rais wa Benki ya Uwekezaji wa Miundombinu ya Asia (AIIB), Bi. Zou Jiayi, pembezoni mwa Mikutano ya Majira ya Kipupwe (Spring Meetings) ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, jijini Washington D.C, nchini Marekani.
Rais wa AIIB, Bi. Zou Jiayi, alisema kuwa Tanzania ni mdau muhimu katika Benki hiyo yenye Makao yake Makuu Beijing nchini China, na kwamba Benki yake imejipanga kuisaidia Serikali kutimiza malengo yaliyopangwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Aliyataja maeneo yenye kipaumbele kuwa ni pamoja na miundombinu ya usafiri wa Reli ya Kisasa, nishati, maji na mawasiliano ambapo kupitia uwekezaji huo, benki hiyo inalenga kuchochea maendeleo ya miundombinu, kupunguza umaskini, kuinua viwango vya maisha ya wananchi na kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), aliikaribisha Benki hiyo kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi ya upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa Mradi wa Reli iendayo kasi-SGR, ujenzi wa Bandari ya Mbegani – Bagamoyo na Bandari za Uvuvi za Zanzibar, Miradi ya kukuza ajira kwa vijana katika sekta ya teknolojia na miradi mingine ambayo pande hizo mbili zitakubaliana.
Waziri wa Fedha, Mhe. Khamis Mussa Omar (Mb) (wa pili kushoto), Rais wa Benki ya Uwekezaji wa Miundombinu ya Asia (AIIB), Bi. Zou Jiayi (Katikati), Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil (Mb) (wa pili kulia), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba (kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Aboud Hassan Mwinyi, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kikao chao kilichofanyika pembezoni mwa Mikutano ya Majira ya Kipupwe (Spring Meetings) ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, jijini Washington D.C, nchini Marekani, ambapo wamejadili kufungua fursa mpya za ufadhili kwa miradi ya kimkakati ya maendeleo, ikiwemo maji, nishati, usafiri, teknolojia ya habari na Mawasiliano pamoja na miundombinu ya kijani.




