Makamu wa Pili wa Rais wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema utakapokamilika ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme cha Matemwe Kusini kitasidia kuondowa changamoto ya upungufu wa nishati ya umeme katika Kisiwa cha Unguja.
Ameyasema hayo mara baada ya kukagua eneo litakalotumika kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa megawats 30 kinachojengwa katika Kijiji cha Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo inayojengwa katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema kumekuwa na upungufu mkubwa wa upatikanaji wa nishati ya umeme jambo linaloleta usumbufu kwa wananchi lakini pia kwa wageni na wawekezaji wanaokuja kuekeza Zanzibar.
Amewaagiza Viongozi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kuhakikisha wanawapa elimu wananchi juu ya ujenzi wa miradi ya maendeleo inayojengwa katika maeneo yao sambamba na kuwafahamisha utaratibu wa ulipwaji wa fidia zao ili kuepuka usumbufu na uharibifu wa miradi hio.
Mhe. Hemed ameiagiza Wizara ya maji kuisimamia vyema miradi hio iweze kukamilika kwa wakati pamoja na kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Kaskazini wanapata huduma ya maji kwa masaa 24 hasa ikizingatiwa kuwa Mkoa huo una uwekezaji mkubwa wa hoteli za kitalii ambazo zina uhitaji mkubwa wa maji.
Amewataka Viongozi na watendaji wa Serikali kuwafikia jamii na kuwasikiliza changamoto zao kwani kufanya hivyo kutapunguza malalamiko kutoka kwa wananchi kwenda serikalini.
katika ziara hio Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed suleiman abdalla amekagua ujenzi wa mradi wa kituo cha kufulia umeme matemwe kusini, mradi wa ujenzi wa barabara ya kijini, mradi wa ujenzi wa uwanja wa mpira kijini, mradi wa ujenzi wa visima vya maji kiashange, mradi wa ujenzi wa tangi la maji nungwi, mradi wa ujenzi wa soko la fungu refu mto wa pwani, mradi wa ujenzi wa dahalia skuli ya donge, mradi wa ujenzi wa kiwanja cha mpira mkoa wa kaskazini unguja panga tupu, mradi wa ujenzi wa barabara ya matetema—mangapwani, pamoja na ujenzi wa barabara ya mto mchanga zingwezingwe.

Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR )Leo tarehe 20 / 04 / 2026




