Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba leo (Jumatatu, Aprili 20, 2026) ameendesha kikao cha kutafuta suluhu ya mgogoro wa Mahomanyika wilayani Dodoma mkoani Dodoma uliodumu kwa karibu miaka 10.
Kikao hicho kilichofanyika Ofisini kwake, Mlimwa jijini Dodoma, kimehudhuriwa na Waziri wa Ardhi, Dkt. Leonard Akwilapo, Naibu Waziri (OWM – TAMISEMI) Dkt. Jafar Seif, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Khatibu Kazungu na uongozi wa Wilaya ya Dodoma na baadhi ya viongozi na wakazi wa Kata za Nzuguni na Ipala.
Kikao hicho ni matokeo ya ziara ya kikazi ambayo Waziri Mkuu aliifanya jana, (Jumapili Aprili 19, 2026) wilayani Chamwino mkoani Dodoma ambapo akiwa katika mkutano wa hadhara katika kata ya Msanga, baadhi ya viongozi na wakazi wa Mahomanyika walieleza kutoridhishwa na utaratibu unaotumika kupima maeneo yao jambo lilowafanya kuwa na mgogoro na Halmashauri ya Jiji la Dodoma.





