Mfilisi wa mali za chama kikuu cha ushirika wa wakulima wa kahawa wilaya ya Mbinga(Mbifacu)Watson Nganiwa,akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Kisare Makori, hati za mali za chama hicho kwenye mkutano mkuu 24 uliofanyika katika ukumbi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga,kulia mwenyekiti wa Mbifacu Michael Kanduyu na kushoto Katibu Tawala wa wilaya ya Mbinga Pendo Daniel(Picha na Muhidin Amri).
Mwenyekiti wa Chama kikuu cha ushirika wa kahawa wilaya ya Mbinga(Mbifacu)Michael Kanduyu,akionyesha hati za mali ya chama hicho kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa 24 uliofanyika katika ukumbi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga jana,kushoto kwake Mkuu wa wilaya ya Mbinga Kisare Makori,wa kwanza kushoto Katibu Tawala wa wilaya hiyo Pendo Daniel(Picha na Muhidin Amri)
Meneja wa Chama kikuu cha ushirika wa kahawa wilaya ya Mbinga Mbifacu Faraja Komba kulia na Mwenyekiti wa Chama hicho Michael Kanduyu katikati,wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Mbinga Kisare Makori baada ya kufungua mkutano mkuu 24 wa Chama hicho uliofanyka jana katika ukumbi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga(Picha na Muhidin Amri).
Mkuu wa wilaya ya Mbinga Kisare Makori klia,akiagana na aliyekuwa mrajisi msaidizi wa ushirika Mkoa wa Ruvuma Peja Mhoja ambaye amehamishiwa Mkoani Tabora,wakati wa mkutano mkuu wa 24 wa Chama kikuu cha ushirika wilaya ya Mbinga Mbifacu uliofanyika jana mjini Mbinga(Picha na Muhidin Amri)
………
Na Mwandishi wetu, Mbinga
VIONGOZI wa vyama vya ushirika wilayani Mbinga,wametakiwa kuwa waaminifu,waadilifu,kufanya kazi kwa weledi, kufuata taratibu za kifedha na kuendelea kusimamia vyema mifumo ya sheria za ushirika ili kuepuka migogoro na upotevu wa rasilimali za vyama vyao.
Kauli hiyo imetolewa jana na mkuu wa wilaya ya Mbinga Kisare Makori,wakati akifungua mkutano mkuu wa 24 wa Chama kikuu cha ushirika wa wakulima wa kahawa(Mbifacu) unaojumuisha wilaya ya Nyasa na Mbinga uliofanyika katika ukumbi wa kanisa katoliki Jimbo la Mbinga.
Makori alisema,mifumo ya ushirika na miongozo ya ushirika inapokiukwa kwa viongozi kufanya watakavyo upelekea kuibuka migogoro na rasilimali za ushirika kupotea,jambo ambalo kwa sasa Serikali isingependa kuona linatokea kwenye sekta muhimu ya ushirika.
Kwa mujibu wa Makori,serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan iingie madarakani imewekeza nguvu kubwa katika kuwahudumia wakulima kupitia ushirika,hivyo ni lazima viongozi wahakikishe wanafanya kazi kwa kuzingitia kanuni,sheria na miongozo ili wakulima walime kwa tija na kuondokana na umaskini kupitia shughuli zao za kilimo.
Makori ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo,amepiga marufuku viongozi wa Amcos kujihusisha kununua kahawa kwa njia zisizo rasmi(magoma) ambayo inawanyima wakulima haki na kuikosesha serikali mapato halisi na takwimu sahihi za uzalishaji.
“Serikali haitafumbia macho na itachukua hatua kali kwa kiongozi yoyote wa ushirika atakayejihusisha na biashara ya magoma,wizi na vitendo vingine vinavyorudisha nyuma jitihada za wakulima na itaendelea kuimarisha sekta ya ushirika ambayo ina mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi yetu”alisema Makori.
Amewataka viongozi wa Amcos kuwa karibu na wakulima ili kutatua changamoto na kusimamia upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima ili wazalishe kwa tija na kujiongezea kipato kupitia kilimo cha zao la kahawa ambalo ni nguvu kuu ya uchumi wa wilaya ya Mbinga.
Meneja wa Mbifacu Faraja Komba alisema,katika msimu 2025/2026 Chama kikuu (Mbifacu)imesimamia makusanyo ya kahawa kutoka kwenye vyama vya msingi vya ushirika jumla ya kilo 23,630,687 za kahawa kavu ambayo ni sawa na punguzo la kilo 416,881 toka kilo 24,047,568 ambazo zilikusanywa 2024/2025.
Alisema,kahawa yote iliyokusanywa kutoka kwa wakulima kupitia vyama vya msingi vya ushirika iliuzwa kupitia minada ya kikanda iliyofanyika Mbinga,Mbeya na Moshi na thamani ya kahawa hiyo ni dola 115,742,140,.41 ambazo ni sawa na fedha za Kitanzania Sh.283,568,244,000.
“katika msimu 2025/2026 chama kikuu kimefanikiwa kukusanya Sh.892,104,402 ambazo zimetoka kwenye vyanzo vikuu viwili ambayo ni miradi ya chama na mapato mengineyo Sh.267,519,403”alisema Komba.
Komba alisema,mapato yaliyotokana na ushuru kutoka vyama vya msingi vya ushirika kwa msimu 2025/2026 Sh.624,584,999 kati ya Sh.678,210,000 na kusimamia usambazaji wa mbolea tani 1,192.2 na katika msimu 2026/2027
chama kimejipanga kuendeleza mradi huo wa pembejeo kupitia fedha za ukomo wa madeni ambazo ni Sh.3,000,000,000.
Naye mwenyekiti wa chama hicho Michael Kanduyu alisema,kuanzishwa kwa vyama vya msingi vya ushirika vinadhoofisha sekta ya ushirika na kuzalisha migogoro kwa wanachama ambao ni wakulima wa zao la kahawa na kuchangia vitendo vya wizi wa mali za wanachama.
Ameiomba serikali,kutoruhusu kuanzishwa kwa vyama vipya badala yake kuimarisha na kusimamia vyama vilivyopo ili viweze kwa manufaa ya ushirika na wakulima.




