Dar es Salaam
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda, ameipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilaya ya Kinondoni kwa usimamizi mzuri wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Gemma yenye urefu wa kilomita 1.78 kwa kiwango cha lami itakayorahisisha shughuli za usafiri na usafishaji na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.
Ameyasema hayo tarehe 17 Aprili, 2026 wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa barabara ya Gemma iliyopo Kata ya Mabwepande, wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam inayojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 3.1 baada ya kukagua na kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo.
Kiongozi huyo ameipongeza TARURA Kinondoni kwa kazi nzuri waliyoifanya inayoakisi dhamira njema ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuwataka kuendelea kudumisha weledi na uadilifu katika usimamizi wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.
Pia, Kiongozi huyo amempongeza Mkandarasi M/s ON Africa Construction Company Ltd kwa kazi nzuri inayofanyika ya utekelezaji wa mradi huo na kumtaka kukamilisha kazi kwa wakati.
Mradi huo unatarajiwa kuboresha miundombinu ya usafiri katika eneo la Mabwepande, kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa wilaya ya Kinondoni.





