Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
Aprili 18, 2026
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Wazo Mwang’onda, amekagua kiwanda cha kutengeneza nguzo za zege cha Coast Concrete Poles kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani na kueleza kuwa ni mwarobaini wa kulinda mazingira kwa kupunguza ukataji miti.
Akizungumza Aprili 18, 2026 wakati Mwenge wa Uhuru ulipopitia miradi nane wilayani Bagamoyo, Mwang’onda alisema uwekezaji huo una mchango mkubwa katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya viwanda nchini.
Alisema ameridhishwa na kazi inayofanywa na wawekezaji wa ndani na kuwahimiza kuongeza juhudi zaidi katika uzalishaji pamoja na kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Nimeambiwa na Mkuu wa Wilaya kuwa mnaongeza kiwanda kingine, hili ni jambo jema kwani nguzo hizi zinahitajika Tanzania na barani Afrika,Msichoke, fanyeni kazi usiku na mchana na tafuteni masoko,” alisema Mwang’onda.
Awali, akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho, Bridget Temba, alisema kampuni hiyo ni tanzu ya DERM Group, iliyoanzishwa mwaka 2018 kupitia ubia kati ya DERM Group na kampuni ya FOSHAN NANHAI kutoka China.
Alisema lengo la mradi huo ni kuzalisha nguzo za zege zinazochangia kuokoa takribani miti 98,000 kwa mwaka, hivyo kusaidia kulinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Bridget alifafanua kuwa uwekezaji wa mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 10, ikiwa ni sehemu ya jitihada za DERM Group kuunga mkono sera ya serikali ya kujenga uchumi wa viwanda.
Aliongeza kuwa kiwanda kina uwezo wa kuzalisha takribani nguzo 266 kwa siku, ambazo hutumika katika miradi ya taasisi za umma ikiwemo Tanesco, TTCL na REA pamoja na sekta binafsi, na hivyo kuchangia kuboresha miundombinu nchini.
“Hadi Machi 2026, jumla ya nguzo 150,000 tayari zimesambazwa,” alisema Bridget.
Vilevile, alieleza kiwanda hicho kimeajiri zaidi ya Watanzania 300 kwa ajira za moja kwa moja, ambapo asilimia 80 ni wakazi wa Bagamoyo.
Alieleza kuwa mradi wa upanuzi wa kiwanda hicho umefikia asilimia 80 na ukikamilika utaongeza uzalishaji kwa asilimia 100, kutoka nguzo 266 hadi 466 kwa siku, pamoja na kuongeza ajira mpya 250.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, alisema jumla ya miradi nane yenye thamani ya shilingi bilioni 11.4 imekaguliwa na mingine kuwekwa mawe ya msingi wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani humo.
Alisema Aprili 19, 2026, Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuendelea na mbio zake katika wilaya ya Chalinze.
Miradi mingine iliyowekwa mawe ya msingi ni pamoja na ujenzi wa jengo la watoto wachanga wanaohitaji uangalizi maalum (NICU), shule ya msingi Sanzale, mradi wa maji Kibosha-Mapinga na ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya sekondari Shushila Ladwa.





