Na Silivia Amandius
Kagera.
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, amewataka viongozi wa vyama vya msingi mkoani Kagera kuongeza juhudi katika kuwapatia wakulima elimu sahihi ya uvunaji wa kahawa iliyokomaa, hatua ambayo imeelezwa kuwa ni muhimu katika kulinda ubora wa zao hilo na kuhakikisha linaendelea kupata soko la uhakika ndani na nje ya nchi.
Sima alitoa wito huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Kido, alipokuwa mgeni rasmi katika mkutano mkuu wa mwaka wa Chama Kikuu cha Ushirika Kagera (KCU 1990), uliofanyika katika Manispaa ya Bukoba April 16, mwaka huu katika ukumbi wa Chama hicho Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe kutoka halmashauri za Muleba, Bukoba na Misenyi.
Katika hotuba yake, Sima alisisitiza kuwa ubora wa kahawa ndio msingi wa ushindani wa zao hilo katika soko la kimataifa. Alieleza kuwa kuvuna kahawa ambayo haijakomaa kunapunguza thamani ya zao hilo na kuathiri mapato ya wakulima pamoja na taifa kwa ujumla. Hivyo, aliwataka viongozi wa ushirika kuhakikisha elimu inawafikia wakulima wote ili kudhibiti changamoto hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa KCU 1990, Bw. Res Mashurano, akiwasilisha taarifa ya mwaka, alisema chama hicho kimeendelea kuimarika kiuchumi. Alieleza kuwa kwa msimu wa 2025/2026, KCU ilikisia kukusanya shilingi bilioni 1.8 kupitia mfuko wa ustawi wa jamii, lakini walifanikiwa kuvuka lengo hilo na kufikia shilingi bilioni 1.873
Mashurano aliongeza kuwa kwa msimu wa 2026/2027, KCU imejiwekea malengo makubwa zaidi ya kukusanya shilingi bilioni 2.05. Ili kufanikisha hilo, chama hicho kinatarajia kukopa kiasi cha shilingi bilioni 20.485 kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) pamoja na taasisi nyingine za kifedha.
Alifafanua kuwa kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 20 zitatumika kununua kahawa kutoka kwa wakulima, huku shilingi milioni 485 zikitengwa kwa ajili ya kuanzisha duka la pembejeo. Hatua hiyo inalenga kurahisisha upatikanaji wa pembejeo bora kwa wakulima na hivyo kuongeza uzalishaji na ubora wa kahawa.
Katika kuonyesha dhamira ya kuinua vijana, Mashurano alisema KCU imetenga shilingi milioni 35.25 kwa ajili ya kufadhili vijana 141 kutoka vyama vya ushirika kusoma mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo vya VETA, ambapo kila chama kitatoa kijana mmoja. Lengo ni kuwawezesha vijana kujiajiri na kuchangia maendeleo ya jamii.
Aidha, KCU imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika kipindi cha mwaka 2025/2026. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa maduka 66 ya biashara katika eneo la Zam Zam kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 884, ukarabati wa jengo kwa ajili ya matumizi ya Benki ya TADB, pamoja na kukamilisha ujenzi wa ukumbi, mfereji na ukuta wa kiwanja cha Rumuli.
Kwa ujumla, mkutano huo umeonesha mwelekeo mpya wa kuimarisha sekta ya kahawa mkoani Kagera kupitia ushirikiano wa serikali na vyama vya ushirika, huku mkazo mkubwa ukiwekwa katika ubora wa zao, uwekezaji na uwezeshaji wa vijana. Hatua hizi zinatarajiwa kuongeza tija kwa wakulima na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa pamoja na taifa kwa ujumla.





