Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema kuwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya barabara utaibadilisha kwa kiasi kikubwa sura ya Jiji la Arusha na kulifanya kuwa kitovu cha kimataifa cha utalii na biashara.
Akizungumza jijini Arusha katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kona ya Mbauda, Waziri Mkuu amebainisha kuwa mafanikio ya utekelezaji wa miradi hiyo yametokana na uongozi thabiti wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amewezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya miradi hiyo mikubwa ya kimkakati.
Ameeleza kuwa miradi hiyo inahusisha ujenzi wa barabara za njia nne, uwekaji wa taa za kisasa za barabarani pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya biashara ikiwemo stendi na masoko ya kisasa. Hatua hiyo inalenga kulifanya Jiji la Arusha kuwa na mwonekano wa kisasa, kuvutia uwekezaji na kuongeza ushindani wake kimataifa.
“Serikali tayari imetoa shilingi bilioni 10.2 kwa ajili ya fidia kwa wananchi waliopisha miradi hiyo, huku mkandarasi akishalipwa malipo ya awali na ujenzi ukiendelea kwa kasi.”amesema .
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, alimshukuru Rais kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi hiyo, akisisitiza kuwa uwekaji wa taa za kisasa utaongeza usalama kwa wananchi. Alifafanua kuwa kila kilometa moja itawekewa taa 40, huku barabara ya Arusha Bypass ikitarajiwa kuwa na zaidi ya taa 1,600.
Aidha, barabara ya Kilombero–Kisongo yenye urefu wa kilometa 9 itapatiwa taa 360 pamoja na kujengewa mitaro mikubwa kwa ajili ya kudhibiti mafuriko, hatua itakayosaidia kulinda miundombinu hiyo na kuboresha usafiri.
Mbunge wa Arusha Mjini, Paul Makonda, amesema miradi hiyo imeleta matumaini mapya kwa wananchi wa Arusha, akieleza kuwa ujenzi wa barabara za kisasa utarahisisha usafiri, kuimarisha usalama na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Awali, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, amesema kuwa mkandarasi wa barabara ya Mbauda–Losinyai hadi Tanganyika Packers alianza kazi Aprili 10, 2026, na mradi huo unatarajiwa kukamilika Aprili 9, 2029. Hata hivyo, kipande cha kilometa 13 kutoka Mbauda hadi Bondeni City kinatarajiwa kukamilika mapema ili kuwanufaisha wananchi.
Ameongeza kuwa jumla ya kilometa 7 zitajengwa kwa kiwango cha njia nne na kilometa 63 kwa kiwango cha njia mbili chini ya mkandarasi China Civil Engineering Construction Company Corporation, ambaye tayari amelipwa malipo ya awali ya shilingi bilioni 17.6.
Vilevile, mradi wa barabara ya Kilombero–Kisongo wenye urefu wa kilometa 9.1 umetangazwa zabuni Aprili 15, 2026, huku ufunguzi wa zabuni ukitarajiwa kufanyika Aprili 30, 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuendelea kuboresha miundombinu ya Jiji la Arusha.
Kwa ujumla, utekelezaji wa miradi hii unatajwa kuwa chachu ya mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Arusha, huku ukiliweka jiji hilo katika nafasi bora zaidi ya ushindani wa kikanda na kimataifa.





