NA DENIS MLOWE, IRINGA
WANANCHI wa Kata ya Lumuli wamejitokeza kwa wingi kushuhudia tukio muhimu la uzinduzi wa gari jipya la wagonjwa (ambulance) lenye thamani ya shilingi milioni 78, lililotolewa na Diwani wa kata hiyo, Abeid Kisinini kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kutoka Reach Out and Touch (ROAT).
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada endelevu za kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.
Uzinduzi huo uliambatana na hamasa kubwa kutoka kwa wakazi wa Lumuli ambao wamesema kuwa kifaa hicho cha usafiri wa dharura kitasaidia pakubwa kukabiliana na changamoto ya usafirishaji wa wagonjwa, hususan kwa rufaa zinazoelekezwa katika hospitali za wilaya na za mkoa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Diwani Abeid Kisinini alisema upatikanaji wa ambulance hiyo unatokana na ushirikiano wa karibu kati yake na wadau wa maendeleo kupitia ROAT.
Alisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa haraka, kwa ubora na bila vikwazo vya usafiri hasa kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya dharura.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Iringa Vijijini, Costantino Kihwele, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM ya Wilaya hiyo, alitoa rai kwa viongozi na wananchi kuhakikisha gari hilo linatunzwa na kutumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa.
Alibainisha kuwa uwepo wa ambulance hiyo ni mchango mkubwa katika kuboresha ustawi wa jamii, na ni hatua inayodhihirisha namna ushirikiano kati ya viongozi na wadau wa maendeleo unavyoweza kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa vijijini.
Kihwele aliongeza kuwa kwa muda mrefu wakazi wa maeneo ya pembezoni, ikiwamo Lumuli, wamekuwa wakikabiliwa na adha ya kusafirisha wagonjwa kwa umbali mrefu bila usafiri wa uhakika. Hivyo, kupatikana kwa gari hilo ni suluhisho litakalopunguza vifo vinavyoweza kuzuilika na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya.
Wananchi waliohudhuria hafla hiyo wameelezea furaha yao huku wakimshukuru Diwani Kisinini na wadau wa ROAT kwa mchango huo muhimu, wakisema kuwa ndio mara ya kwanza kupokea huduma ya aina hiyo ndani ya kata yao.




