Mwenyekiti wa TAMWA Dr Kaanaeli Kaale wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka leo April 17

Baadhi ya wanachama wa chama cha waandishi wa habari wanawake TAMWA walioshiriki katika mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho.

Mkuu wa idara ya operesheni na tathimini kutoka mfuko wa fidia kwa wafanyakazi WCF wakati akiwajengea uelewa wanachama wa TAMWA
Na Neema Mtuka, Dar es Salaam
Waandishi wa habari wametakiwa kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ili iwasaidie wanapokumbana na changamoto mbalimbali wanapotekeleza shughuli zao za kila siku.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Idara ya Operesheni na Tathmini kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Amri Kombo, katika mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) unaofanyika kwa siku mbili kuanzia Aprili 17–18, 2026 katika ofisi za chama hicho, Sinza Mori jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia mfuko huo, Kombo amesema kwa sasa mfuko huo unatoa mafao mbalimbali ikiwemo fao la utegemezi, pamoja na mafao ya ulemavu wa kudumu na wa muda mfupi.
Aidha, amesisitiza kuwa wanachama wa TAMWA, taasisi na kampuni wanapaswa kujiunga na mfuko huo ili waweze kunufaika na huduma zake, akieleza kuwa mfuko huo unagusa moja kwa moja maisha ya wafanyakazi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAMWA, Dkt. Kaanaeli Kaale, wakati akifungua mkutano huo, amewataka waandishi wa habari kuandika habari zenye tija na zinazochochea maendeleo ya jamii.
Baadhi ya wadau walioshiriki katika mkutano huo na kutoa elimu ni pamoja na NSSF, WCF, Orbits Security na UTT-AMIS, ambao waliwahimiza wanachama kujiunga na mifuko hiyo ili kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wao, baadhi ya wanachama walioshiriki katika mkutano huo, akiwemo Cresensia Daimon, wameishukuru TAMWA pamoja na wadau kwa mafunzo yaliyotolewa, wakisema yamewaongezea maarifa na kuwajengea uelewa kuhusu mifuko hiyo.



