NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Mabingwa Watetezi Yanga Sc imeendelea kuwa tishio katika Ligi Kuu Bara ikishusha kipigo kingine kikali msimu huu, ikiichapa Mbeya City kwa mabao 6-0, huku ikiandika rekodi mbili.
Ushindi huo wa Yanga ikiwa nyumbani, unaifanya kuendelea kutamba juu ya msimamo wa ligi hiyo ikifikisha pointi 47 baada ya kucheza mechi 19.
Wafungaji wa mabao katika mechi hiyo iliyochezwa leo Alhamisi Aprili 16, 2026 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar, ni Pacome Zouzoua, Prince Dube ambao kila mmoja aliweka wavuni mabao mawili, mengine yakifungwa na Maxi Nzengeli na Mohammed Hussein ‘Tshabalala.
Yanga imeweka rekodi ya kwanza ikiwa ndio timu iliyopata ushindi mkubwa msimu huu wa mabao sita, ikifanya hivyo mara ya pili baada ya awali kuichapa Mashujaa, Januari 19, 2026.
Rekodi ya pili ya Yanga iliyoandika kwenye ushindi huo ni kuwa timu iliyoipiga kipigo kikali Mbeya City bila ya majibu, iliyopoteza 6-0 kwa mara ya kwanza tangu timu hiyo ianzishwe.
Mara ya mwisho City ambayo haipo kwenye kiwango kizuri msimu huu kupoteza vibaya ilikuwa Desemba 31, 2022 ilipochapwa 6-1 dhidi ya Azam FC ugenini.
Yanga imeipeleka City eneo gumu ikiwa timu nyingine iliyoruhusu mabao mengi, sawa na KMC ambapo zote zimefungwa mabao 30 kila moja ndani ya ligi hiyo msimu huu.
Mbeya City kipigo hicho imefanya kuendelea kusalia nafasi ya 13 katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 17 baada ya kucheza mechi 19. Chini yake kuna Fountain Gate (pointi 16), Tanzania Prisons (pointi 14) na KMC (pointi 9).




