Farida Mangube, Morogoro
Serikali kupitia Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) imeendelea kuimarisha uhifadhi wa misitu na maendeleo ya jamii kwa kutoa ruzuku zinazolenga
kukuza miradi endelevu ya mazingira na uchumi wa kijani.
Hayo yamebainishwa katika ufunguzi wa mafunzo kwa wanufaika wapya wa ruzuku kwa mwaka wa fedha 2025/2026 yaliyofanyika Morogoro, yakikutanisha wanufaika, waratibu wa miradi, maafisa misitu pamoja na maafisa nyuki kutoka mikoa yote nchini.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TaFF, Dkt. Tuli Salum Msuya, alisema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wanufaika katika kusimamia na kutekeleza miradi yao kwa ufanisi, hususan katika usimamizi wa fedha za ruzuku, utekelezaji wa mikataba pamoja na uandaaji wa taarifa za maendeleo ya miradi.
Alisema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka kipaumbele katika sekta ya misitu kama mhimili muhimu wa uhifadhi wa mazingira, kuongeza uzalishaji na kukuza sekta ya utalii kupitia misitu endelevu.
Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, jumla ya miradi 137 imeidhinishwa kupatiwa ruzuku kati ya zaidi ya maombi 400 yaliyowasilishwa, ambapo miradi hiyo inatekelezwa katika wilaya zaidi ya 40 nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Miradi na Mipango TaFF, Johnny Richard Mbwambo, alisema mpaka sasa TaFF imetoa shilingi bilioni 70 kuwezesha miradi ya misitu na ufugaji nyuki, hatua iliyochangia upandaji miti katika mashamba zaidi ya 290 pamoja na kuimarisha uhifadhi wa maeneo makubwa ya misitu nchini.
Mbwambo aliongeza kuwa awali baadhi ya changamoto zilijitokeza katika matumizi ya fedha na utoaji wa taarifa, hali iliyosababisha kuanzishwa kwa mafunzo kabla ya utekelezaji wa miradi ili kuongeza uwajibikaji na ufanisi.
Kwa upande wao, wanufaika wa ruzuku hiyo walisema mafunzo hayo yamewasaidia kupata uelewa mpana kuhusu usimamizi wa miradi na matumizi sahihi ya fedha za ruzuku, huku wakisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa ushirikiano na kuhakikisha fedha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Kwa sasa, takriban vikundi 79 vinanufaika na miradi inayofadhiliwa na TaFF, ikiwemo shughuli za kilimo na ufugaji nyuki zinazochangia uhifadhi wa misitu ya asili.





