Zaidi ya wananchi 700,000 kutoka kata 19 katika Mkoa wa Geita wanatarajiwa kunufaika na mradi mkubwa wa maji unaogharimu zaidi ya Sh bilioni 124, utakaoboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Geita Vijijini.
Mradi huo unatarajiwa kuanza kutoa huduma ifikapo Septemba 30, 2026, ukiwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 45 za maji kwa siku, hatua inayolenga kumaliza changamoto ya uhaba wa maji katika maeneo husika.
Akizungumza Aprili 16, 2026 wakati wa ukaguzi wa mradi huo katika Kata ya Senga, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, amesema mradi huo ni sehemu ya miradi 28 ya maji inayotekelezwa nchi nzima kwa lengo la kuboresha huduma hiyo muhimu.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii, huku ukisaidia kuvuka malengo ya Serikali ya kuhakikisha upatikanaji wa maji unafikia asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijijini, na badala yake kufikia huduma kwa asilimia 100.
“Tumeshuhudia miradi mingi, lakini huu ni miongoni mwa miradi mikubwa na yenye tija kubwa. Nawapongeza viongozi, wataalamu na wasimamizi kwa weledi na usimamizi mzuri wa mradi huu,” amesema Kihongosi.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Geita (GEUWASA), Mhandisi Frank Changawa, amesema mradi huo unagharimu dola za Marekani milioni 53.463 na hadi sasa umefikia asilimia 80 ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu yake.





