Na Mwandishi Wetu, Pwani
Uhifadhi wa misitu katika Halmashauri ya Chalinze, mkoani Pwani, umeanza kuzaa matunda yanayoonekana wazi, baada ya uharibifu wa misitu kupungua kwa kiwango kikubwa huku ushiriki wa wananchi ukiongezeka na fursa za kipato mbadala zikitanuka kwa kasi.
Mafanikio hayo yanachochewa na utekelezaji wa mradi wa Building the Resilience of Forest Biodiversity to the Threats of Climate Change (BUREFOBI-NFR) unaotekelezwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP).
Akizungumza leo Aprili 15, 2026 wakati wa ziara ya tathmini ya mradi huo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze, Archanus Kilaja, alisema mafanikio hayo ni matokeo ya mshikamano wa dhati kati ya serikali, wadau wa maendeleo na jamii.
“Ushirikiano huu umejenga msingi imara wa kulinda misitu yetu na kuhakikisha rasilimali hizi zinakuwa chachu ya maendeleo endelevu kwa wananchi,” alisema Kilaja.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi huo, Mhifadhi Mkuu wa TFS, Someni Mteleka, alifafanua kuwa lengo kuu ni kuimarisha uhifadhi wa misitu sambamba na kuongeza uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Katika utekelezaji wake, mashirika ya kijamii nayo yamekuwa na mchango mkubwa. Afisa kutoka MJUMITA, Benedict Minda, alisema kupitia mradi huo vijiji sita vimewezeshwa kutenga na kusimamia misitu yao kwa kutumia mipango shirikishi na sheria ndogo ndogo.
Alivitaja baadhi ya vijiji hivyo kuwa ni Kimange, Mbwawa, Msanja na Kwarombo, ambapo jumla ya hekta 1,077.27 zimetengwa kwa ajili ya misitu ya vijiji.
“Tofauti na ilivyokuwa awali, sasa kuna doria za mara kwa mara, utekelezaji wa sheria umeimarika na uelewa wa jamii kuhusu uhifadhi umeongezeka kwa kiasi kikubwa,” alisema Minda.
Naye Mhifadhi wa Msitu wa Mazingira Asili wa Uziguwa, Jonathan Mpangala, alisema hatua hizo zimewezesha vijiji vinne kuanzisha jumla ya hifadhi za misitu ya vijiji 17 zenye takribani hekta 4,077.27.
Mbali na uhifadhi, mradi huo umefungua milango ya uchumi kwa wananchi kupitia shughuli mbadala kama kilimo cha mihogo na nyanya pamoja na upandaji miti.
“Wananchi waliokuwa wanategemea ukataji miti na uchomaji mkaa sasa wanapata kipato halali kupitia kilimo na shughuli nyingine rafiki kwa mazingira,” alisisitiza Mpangala.
Wataalamu wa mazingira wanasema mafanikio hayo ni hatua muhimu katika kuhakikisha uendelevu wa rasilimali za misitu nchini, huku yakitoa mfano wa kuigwa kwa maeneo mengine yenye changamoto kama hizo.





