Na Maelezo Zanzibar 13.04.20256
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini Joseph J. Kilangi, amesema Serikali inaendelea kuweka miundombinu bora ya maji safi na salama ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo muhimu kwa uhakika.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya sekta ya maji katika Mkoa wa Mjini Magharibi, kupitia mradi wa upanuzi wa maji wa EXIM, Kilangi amesema mradi huo unalenga huduma ya maji inawafikia wananchi wote.
Ameeleza kuwa katika kipindi cha masika, magonjwa ya mlipuko huongezeka yakiwemo kipindupindu, hali inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa maji safi na salama.
“Maradhi ya kipindupindu husababishwa na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa maji safi na salama” amesema Katibu.
Katibu Kilangi amebainisha kuwa maeneo ya Kilimahewa yameripotiwa kuwa na maambukizi ya kipindupindu, hivyo kusisitiza umuhimu wa kukamilisha uwekaji wa miundombinu ya maji ili kudhibiti mlipuko huo, hasa wakati wa mvua za masika.
Aidha, amesema ujenzi wa miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali umeathiri vyanzo na miundombinu ya maji, na kusababisha wananchi wengi kukosa huduma hiyo hivyo Serikali imetenga fedha na vifaa kusaidia Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kurejesha huduma kwa wananchi.
“Tunaendelea kusaidia mamlaka ya maji kwa kuweka vifaa ili kuhakikisha tunasambaza na kulaza mabomba mapya katika maeneo yote yaliyoharibika kutokana na ujenzi wa barabara,” amefafanua.
Vilevile, amewataka watendaji wa ZAWA kuendelea kufufua visima vya maji, akibainisha kuwa hadi sasa visima vitano vimefufuliwa ili kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo.
Aidha, amewahimiza masheha na madiwani kuimarisha ulinzi wa vyanzo vya maji ili kuhakikisha vinatunzwa na kudumu.
Katibu Kilangi amewataka wananchi kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kuboresha huduma hiyo, akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha Mkoa wa Mjini Magharibi unapata maji ya kutosha, safi na salama pamoja na kuwahamasisha wananchi kuchangia huduma hiyo kwa kulipa gharama nafuu.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Upanuzi wa Huduma ya Maji kutoka Rand Water Zanzibar (ZAWA) Shoumbanah Saleh Mohamed, amesema mradi huo unalenga kurejesha huduma ya maji ambayo imekosekana kwa muda mrefu kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara.
Nae, Diwani wa Wadi ya Kijitoupele Saleh Yahya Saleh, ameahidi kushirikiana na wananchi kulinda miundombinu ya maji na kuwataka waache kujenga katika maeneo ya vyanzo vya maji ili kuepusha uharibifu.
Katibu Mkuu huyo ametembelea maeneo mbali mbali kam vile Kilimahewa, Bumbwisudi, Mtoni na Kidutani kwarara maeneo hayo yameanza utekelezaji wa mradi huo ambapo Bumbwisudi wanananchi 430 watanufaika, Kilimahewa wananchi 286 na Kidutani Kwarara wananchi 756 wataweza kuunganishiwa huduma ya maji safi na salama.





