…………
NA DENIS MLOWE. IRINGA 
SERIKALI imesema ina mpango wa kufanya ukarabati na maboresho katika skimu ya umwagiliaji ya Mkoga Chelahani iliyopo Kata ya Isakalilo, Iringa Mjini, ili kuongeza uzalishaji na kupanua ajira kwa maelfu ya wakazi wanaoitegemea kwa shughuli za kilimo.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni baada ya Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhil Ngajilo, kutaka kufahamu ni lini Serikali itatekeleza ukarabati wa skimu hiyo ambayo imekuwa chanzo muhimu cha kipato kwa zaidi ya watu 10,000.
Ngajilo alisema skimu hiyo ni miongoni mwa eneo linalochochea uchumi wa wananchi wa Iringa Mjini, lakini imekuwa ikikabiliwa na changamoto za miundombinu chakavu zinazoathiri ufanisi wa uzalishaji.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde alisema Serikali inatambua umuhimu wa skimu hiyo na tayari imepanga kuanza maboresho yatakayowezesha wakazi wa eneo hilo kufanya kilimo kwa ufanisi zaidi.
Alisema maboresho hayo yamelenga kuongeza tija, kupunguza adha kwa wakulima na kuifanya skimu hiyo ichangie kikamilifu katika kukuza uchumi wa wananchi wa Iringa.
“Wananchi wa Iringa Mjini waondoe wasiwasi. Serikali tuko tayari kuboresha na kukarabati skimu ya Mkoga Chelahani ili izalishe zaidi na iendelee kutoa ajira kwa wananchi,” alisema Naibu Waziri.
Kwa miaka mingi skimu hiyo imekuwa ikitumika kuzalisha mazao mbalimbali ikiwemo mbogamboga, mpunga na mazao ya biashara, ambayo yanatajwa kuchangia kwa kiwango kikubwa kipato cha kaya na ajira kwa vijana wa eneo hilo.