Mkuu wa wilaya ya Tunduru Denis Masanja katikati aliyevaa kaunta suti,akikata utepe kuzindua magari ya Chama kikuu cha ushirika wilaya ya Tunduru(TAMCU LTD)magari hayo ni sehemu ya miradi  ambayo itakiezesha chama hicho kuongeza mapato yake.

Baadhi ya magari(malori) ya Chama Kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma(TAMCULTD) yaliyonunuliwa na Chama hicho kwa ajili ya kubeba mazao yakiwemo ufuta kwa ajili ya kupelekwa kwenye minada.

……………..

Na Mwandishi Wetu, Tunduru

CHAMA kikuu cha ushirika wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma(TAMCU LTD),kimepanga kukusanya na kuuza ufuta wa wakulima  zaidi ya tani 7,500 katika msimu wa kilimo 2026/2027,hivyo kuvuka lengo la uzalishaji ikilinganisha na msimu  2025/2026 ambapo kilikusanya  na kuuza jumla ya tani 5,047.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mwenyekiti wa Chama hicho Mussa Manjaule,wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu maandalizi ya minada ya zao la ufuta inayotarajiwa kuanza mwezi mei  ofisini kwake mjini Tunduru.

Manjaule alisema,katika msimu 2026/2027 Chama hicho kimewafikia wakulima wengi na kuwahamasisha kupanua mashamba pamoja na kugawa mbegu bora za ufuta zaidi ya tani 16 bure ili kuwawezesha  kulima kwa tija na kuongeza uzalishaji.

“Tuna uhakika mbegu tulizotoa  msimu huu zimewasaidia sana wakulima,ndiyo maana ukienda mashambani hali ni nzuri,tuna amini uzalishaji wa zao la ufuta mwaka huu utakuwa mkubwa ikilinganisha na msimu uliopita ambao tulizalisha tani 5,047 tu”alisema Manjaule.

Manjaule,amewataka wakulima kuendelea na maandalizi kwa kuhakikisha wanazingatia kanuni bora za ili wapate ufuta mzuri ambao utakubalika sokoni kupitia minada  mbalimbali.

Manjaule,amewatoa hofu wakulima kuhusu changamoto ya soko la uhakika,ambapo amewahakikishia kuwa,mwaka huu watarajie kupata fedha nyingi kwani wanunuzi wameonyesha kuhitaji ufuta wote utakaozalishwa  msimu huu.

Kwa upande wake Meneja wa Chama  kikuu cha ushirika Tamcu Marcelino Mrope alisema,kuelekea msimu wa  mauzo wa mazao mchanganyiko  hususani ufuta na mbaazi tayari wamepata viroba(mifuko)  laki tatu kwa ajili ya kukusanya na kuhifadhi ufuta kutoa kwa wakulima.

Mrope alisema,mifuko hiyo itatosheleza kwani mahitaji halisi  ni mifuko laki moja na elfu hamsini(150,000)ambayo itawezesha kukusanya na kuuza ufuta tani 7,500 utakaozalishwa katika msimu wa kilimo 2026/2027.

“ kwa hiyo hapa unaona   msimu huu tuna ziada mara mbili ya mahitaji yetu,tumejipanga vizuri na wakulima wetu wasiwe na hofu  kuhusu uhaba wa mifuko kwa ajili ya kukusanya ufuta watakaozalisha,dhamira yetu ifikapo mwezi wa tano kuanza minada ya kwa zao la ufuta”alisema Mrope.

Alisema, katika msimu huu wa mauzo wamejipanga kuhakikisha wakulima wanapata soko la uhakika na serikali kupitia mfumo wa soko la bidhaa Tanzania(TMX) itaendeleao kusimamia soko la mazao yote yatakayouzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umekuwa na manufaa makubwa kwa wakulima tangu ulipoanzishwa.

Mrope,amewakumbusha wakulima wote,kuhakikisha wanatumia vyama vya msingi vya ushirika(Amcos)kuuza ufuta na mazao yote ya kimkakati na kuepuka kuuza kwa walanguzi walioanza kupita mashambani wakishawishi wakulima wauziwe ufuta kwa bei ndogo isiyolingana na gharama ya  uzalishaji.

Alisema,Chama kikuu kitawalipa wakulima fedha zao  kwa wakati kama  ilivyofanya kwenye zao la korosho na mazao mengine yanayouzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ndani ya siku tatu baada ya kufanyika kwa mnada.

“nawaomba  wakulima wetu wote waachane kabisa na walanguzi wanaopita kwenye maeneo yao,tunataka faida inayopatikana iwafikie moja kwa moja na fedha hizo ziingie kwenye mzunguko katika wilaya yetu ya Tunduru na Mkoa wa Ruvuma”alisema Mrope.