Simba SC imeshindwa kupunguza pointi dhidi ya vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga, baada ya kubanwa mbavu ya kutoka sare tasa na TRA United, katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara uliopigwa leo katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Kufatia matokeo hayo imeifanya Yanga kuzidi kukaa kileleni wakiwa na pointi 44, ikiwaacha wekundu hao wa Msimbazi wakiwa na pointi 36 ikikamata nafasi ya pili.
Katika mchezo huo Simba ilianza dakika 45 za kipindi cha kwanza ikijaribu kusaka bao la mapema, lakini TRA United ilionekana kuwa bora katika kulinda ikiongozwa na nahodha, Nassry Kombo huku ikitumia idadi kubwa ya viungo, akiwemo Jamali Dulazi, Chanda Chewe na Ally Ng’anzi kudhibiti presha ya mshambulizi ya wekundu hao wa Msimbazi.
Kocha wa TRA United, Etienne Ndayiragije, alionekana kuingia na mpango mzuri ambapo wachezaji wake waliongeza presha ya kutafuta mpira mara tu wanaposogea katika nusu ya pili ya uwanja kwa kutumia muundo ya pembe tatu.
Tofauti na ilivyokuwa katika mechi tano zilizopita za Simba dhidi ya TRA, mechi ya leo vijana wa Steve Barker walishindwa kupata bao katika dakika 45 za kipindi cha kwanza. TRA United ilikuwa ikiwasubiri na baada ya kunasa mpira ilitumia kasi ya wachezaji wake wa pembeni akiwemo Ramadhan Chobwedo katika mashambulizi ya kustukiza.
Simba ilirejea kipindi cha pili na kujaribu kuifungua ngome za TRA, baada ya dakika 14 za kipindi cha pili ikifanya mabadiliko mawili kwa mpigo, ilimtoa kiungo wa kati, Alassane Kante na winga Libasse Guaye huku wakiingia Clatous Chama na Morice Abraham ili kuongeza nguvu katika eneo la mwisho.
Hata hivyo, TRA United iliendelea kucheza kwa nidhamu ya kujilinda huku katika kipindi hicho cha pili ikionekana kuwa na idadi kubwa zaidi ya wachezaji nyuma tofauti na kipindi cha kwanza ambapo ilikuwa na ukuta wa wachezaji wanne, akiwemo Kombo na Mganda, Christopher Tebandeke ambaye alimpa wakati mgumu, Seleman Mwalimu.
Dakika ya 77, Simba ilifanya mabadiliko ya tatu katika mchezo huo kwa kumtoa Neo Maema na kuingia Inno Loemba, kisha dakika ya 84 ikafanya mabadiliko mengine kwa kuwatoa Shomary Kapombe na Mwalimu, wakaingia David Kameta ‘Duchu’ na Hussein Mbegu.
TRA United ilijikuta ikimaliza pungufu katika mchezo huo kufuatia Nouma kuonyesha kadi ya pili ya njano dakika ya 88 iliyozaa nyekundu. Kadi ya kwanza alionyeshwa dakika ya 82, mpaka dakika ya 90 ya mchezo hakuna timu iliyopata bao.




