KATIBU wa UWT Wadi ya Mwanakwere Ndugu Khadija Seif akisoma Taarifa ya Utendaji wa Majukumu mbali mbali ya Wadi hiyo mara baada ya kufunguliwa kwa Kikao hicho cha Baraza la UWT ngazi ya Wadi huko katika Ukumbi wa Mikutano wa Tawi la Mwanakwerekwe ‘A’.
BAADHI ya Viongozi wa UWT Ngazi ya Mkoa na Jimbo wakiwa katika Kikao hicho cha Baraza la UWT Wadi ya Mwanakwerekwe.
MWENYEKITI wa UWT Mkoa wa Magharibi Unguja Ndugu Zainab Ali Maulid,akiwahutubia Wajumbe wa Baraza la UWT Wadi ya Mwanakwerekwe mara baada ya kufungua Kikao cha Baraza hilo kwa niaba ya Wadi 14 za UWT za Wilaya ya Dimani zilizofanya Vikao leo Tarehe 16/06/2019.
MJUMBE wa Baraza la UWT Wadi ya Mwanakwerekwe ambaye pia ni Mwakilishi wa Viti Maalum Mhe.Mwanaidi Kassim Mussa akitoa maoni yake kuhusu Taarifa ya utekelezaji iliyowasilishwa na Wadi hiyo.
WAJUMBE wa Baraza la UWT Wadi ya Mwanakwerekwe wakisikiliza nasaha zinazotolewa na Viongozi wao kupitia Kikao hicho.
*******************************
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Tanzania Mkoa wa Magharibi Unguja Ndugu Zainab Ali Maulid, amezitaka Ngazi za Wadi ndani ya Mkoa huo kufanya Vikao vya Kawaida na Kikatiba kwa Mujibu wa Miongozo ya Katiba na Kanuni ya Umoja huo.
Wito huo aliutoa wakati akiwahutubia Wajumbe wa Baraza la UWT Wadi ya Mwanakwerekwe katika Mkutano wa Baraza hilo, uliofunguliwa kwa niaba ya Mikutano yote iliyofanyika leo ya Mabaraza 14 yaliyopo katika Wilaya ya Dimani Unguja.
Alisema ufanisi wa kiutendaji ndani ya Umoja huo inatokana na Utekelezaji wa maelekezo ya Vikao halali vinavyotoa maazimio na maelekezo ya utatuzi wa Changamoto mbali mbali zinazowakabili Wanachama,Viongozi na Watendaji wa UWT.
Alisema Vikao ndio sehemu pekee ya kujitathimini na kupanga mikakati ya Utendaji wa shughuli mbali mbali za UWT hasa katika wakati wa sasa wa kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Dola wa Mwaka 2020.
Alisema kila Mwanamke ndani ya Umoja huo anatakiwa kuwahamasisha Wanawake wengine hasa waliokuwa hawajajiunga na UWT na CCM kuweza kujiunga ili wanufaike na Siasa Bora zinazoendeshwa na Chama Cha Mapinduzi.
Mwenyekiti huyo aliwakumbusha Akina Mama hao kwamba wanatakiwa kujipanga vizuri juu ya kuwahamasisha Wanawake kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura pindi wakati wa zoezi hilo utakapofika.
Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo Zainab, aliwasisitiza Wanawake hao kushiriki katika harakati za kukemea na kupambana na Vitendo vya Udhalilishaji wa Kijinsia kwani vinakwamisha malengo ya Vijana hasa wa Kike.
Naye Mwenyekiti wa Wadi hiyo, Ndugu Amina Khalfan alisema watayafanyia kazi kwa vitendo maelekezo yote yaliyotolewa na Mwenyekiti huyo kwa lengo la kuimarisha shughuli mbali mbali za Umoja huo katika Wadi hiyo.
Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza hilo ambaye pia ni Mwakilishi wa Viti Maalum Mhe.Mwanaidi Kassim Mussa aliwashauri Viongozi wa Wadi hiyo kuendelea kuwa Wabunifu na kushirikiana na Viongozi mbali mbali wa ngazi za juu za Umoja huo ili wasaidie kutatua kwa haraka changamoto zinazowakabili.