Na Silivia Amandius
Kagera.
Mhandisi Tawakal Rwahila, Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kagera, amesema kuwa mradi wa upanuzi wa kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Kibeta umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 30 mwaka huu.
Kituo hicho kilijengwa mwaka 1993 kikiwa na uwezo wa megawati 20, lakini kutokana na ongezeko kubwa la mahitaji ya umeme kwa wananchi na shughuli za kiuchumi, Serikali ilianza rasmi mradi wa upanuzi mwaka 2023 kwa lengo la kuongeza uwezo hadi kufikia megawati 120.
Akieleza maendeleo ya mradi huo, Mhandisi Rwahila amesema tayari vifaa muhimu vimewasili na vinaendelea kufungwa, ikiwa ni pamoja na vivunja umeme (circuit breakers) vya kisasa, njia ya ziada ya usambazaji (feeder), pamoja na transfoma inayopunguza msongo wa umeme kutoka kilovolti 33 hadi kilovolti 11.
Ameongeza kuwa kwa sasa majaribio ya awali ya mfumo yanaendelea, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kukamilika kwa mradi huo kwa wakati uliopangwa.
Mradi huo unatekelezwa na mkandarasi TBEA kutoka nchini China, ambaye anaendelea na usimikaji wa miundombinu kwa viwango vinavyolenga kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya umeme katika mkoa wa Kagera.
Kwa mujibu wa Mhandisi Rwahila, kukamilika kwa kituo hicho kutaongeza uwezo wa usambazaji wa umeme pamoja na kupunguza changamoto ya ukatikaji wa umeme katika wilaya za Bukoba, Missenyi na Muleba.
Aidha, amesema katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025, TANESCO imefanikiwa kusambaza umeme katika vijiji vyote 664 vya mkoa wa Kagera, huku zaidi ya vitongoji 3,000 tayari vikiwa vimeunganishwa na huduma hiyo.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha umeme unafika hadi ngazi ya vitongoji, na mradi huu wa Kibeta ni sehemu muhimu ya kufanikisha azma hiyo,” amesema Rwahila.
Ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia mkoa wa Kagera kupata umeme wa kutosha, huku ukifungua fursa mpya za uwekezaji hususan katika sekta ya viwanda, biashara na kuongeza ajira kwa wananchi.




