Na.Sophia Kingimali.
Wakati dunia ikiendelea kukabiliwa na ongezeko la taka, Tanzania imeanza kuchukua hatua madhubuti kubadili changamoto hiyo kuwa fursa ya kiuchumi kupitia mkakati mpya wa kitaifa wa usimamizi wa taka wa mwaka 2025–2030.
Kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), serikali inaelekeza nguvu katika dhana ya uchumi rejeshi—mfumo unaolenga kupunguza taka na kuzigeuza kuwa rasilimali zenye thamani.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Taka Sifuri yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema ni wakati wa sekta binafsi kuchangamkia uwekezaji katika teknolojia za kisasa za kuchakata taka.
Amesisitiza kuwa badala ya taka kuwa mzigo kwa mazingira, zinaweza kuwa chanzo cha malighafi kwa viwanda, ajira kwa vijana na kichocheo cha uchumi wa viwanda endapo zitasimamiwa kwa ufanisi.
Kauli mbiu ya mwaka huu ya “Kuwezesha Taka Sifuri Kwenye Sekta ya Chakula” inaweka mkazo katika kupunguza upotevu wa chakula, huku kauli mbiu ya kitaifa ya “Taka ni Fursa” ikihamasisha mabadiliko ya fikra miongoni mwa wananchi.
Hata hivyo, pamoja na jitihada hizo, takwimu zinaonesha ukubwa wa changamoto iliyopo.
Tanzania huzalisha zaidi ya tani milioni saba za taka ngumu kila mwaka, lakini ni chini ya nusu pekee inayokusanywa ipasavyo. Sehemu kubwa ya taka husalia kwenye mazingira, ikiathiri mifumo ya maji na afya ya jamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware, anasisitiza kuwa suluhisho halipo tu kwenye sera bali pia kwenye mabadiliko ya tabia za wananchi ambapo anabainisha kuwa taka za chakula zinaweza kuzalisha mbolea na nishati, plastiki kurejelezwa kuwa bidhaa mpya, na vyuma chakavu kuingia tena kwenye mnyororo wa uzalishaji.
Lengo la maadhimisho hayo ni kutoa ujumbe kwa wananchi ya kuwa vita dhidi ya taka si jukumu la serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi kuanzia majumbani hadi viwandani kubadili mtazamo na kuona taka kama rasilimali badala ya uchafu.

