Na Silivia Amandius
Muleba.
Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na MNEC Taifa, Ndg. Kenani Kihongosi, ameipongeza serikali pamoja na TANROADS mkoa wa Kagera kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa daraja la kamishango lililopo halmashauri ya wilaya ya Muleba lenye thamani ya shilingi bilioni 12.5, akisema ni hatua muhimu katika kuboresha miundombinu na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi
Akizungumza wakati wa ziara yake iliyofanyika Machi 27, 2026, Meneja wa TANROADS mkoa wa Kagera, Mhandisi Samwel Mwambungu, amesema kuwa jumla ya shilingi bilioni 12.5 zimetumika katika ujenzi wa daraja hilo pamoja na uboreshaji wa miundombinu inayolizunguka, ikiwemo uwekaji wa taa za barabarani 56 zinazotarajiwa kusimikwa. Amesema daraja hilo lina ubora wa juu na upana unaoruhusu magari kupishana kwa urahisi tofauti na daraja la awali lililokuwa finyu na kusababisha changamoto kubwa kwa watumiaji wa barabara.
Mhandisi Mwambungu amesema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo mbele ya viongozi mbalimbali, akibainisha kuwa mradi huo unatekelezwa na mkandarasi mzawa. Ameongeza kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutachochea ukuaji wa uchumi katika eneo husika kwa kuimarisha mnyororo wa thamani pamoja na kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.
Kwa upande wake, Ndg. Kihongosi ametoa pongezi kwa TANROADS na chama kwa ujumla kwa kuendelea kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo, akisema kuwa miradi hiyo inaondoa changamoto kwa wananchi. Aidha, amemtaka mkandarasi kukamilisha mradi huo kwa haraka ili ufunguliwe na kuanza kutumika mapema, huku akiipongeza halmashauri kwa usimamizi mzuri wa mradi huo na kueleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa.
Katika hatua nyingine, Kihongosi amewataka wananchi kuendelea kulinda na kutunza miundombinu hiyo, hususan taa za barabarani, akieleza kuwa kumekuwa na matukio ya wizi wa vifaa hivyo.
Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na upendo miongoni mwa wananchi ili kuhakikisha miradi hiyo inadumu na kuwanufaisha wote.
Nao baadhi ya wananchi, akiwemo Bi Spenzioza Protazi na Bw. Abdurashid Yunusu, wameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kutekeleza mradi huo, wakisema kuwa hapo awali walikumbwa na changamoto ya magari kukwama pamoja na daraja kujaa maji wakati wa mvua kutokana na udogo wa daraja la zamani.
Wamesema daraja hilo jipya ni chachu ya maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo na kuwataka wananchi wenzao kulinda mradi huo kwa umakini.

