MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, ametoa taarifa rasmi kwa wanahabari kuhusu maandalizi na ratiba ya mazishi Aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Marehemu William Vangimembe Lukuvi.
Akizungumza mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa marehemu eneo la Gangilonga, James aliwapa pole wananchi na kusisitiza kuwa msiba huo ni pengo kubwa kwa Iringa na Taifa kwa ujumla.
Amesema kuwa mwili wa marehemu unatarajiwa kuwasili mkoani Iringa tarehe 29 saa 11 jioni kupitia uwanja wa ndege wa Nduli, ambako utapokelewa rasmi na kuelekezwa moja kwa moja nyumbani kwake Gangilonga. Wananchi, ndugu, jamaa na marafiki watapata nafasi ya kuuona na kutoa heshima za mwisho.
Tarehe 30 asubuhi, kutafanyika ibada ya kumuombea marehemu katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Kihesa, ambako wananchi watajumuika kutoa heshima za mwisho. Saa 9 alasiri siku hiyo, mwili utaondolewa kutoka parokia hiyo kuelekea kijiji cha Idodi, ambapo utapokelewa saa 11 jioni na kulazwa nyumbani kwake.
Mazishi ya kitaifa yanatarajiwa kufanyika tarehe 31 katika kijiji cha Idodi, Jimbo la Ismani, Halmashauri ya Iringa DC. James amesema mazishi hayo yataongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, pamoja na viongozi mbalimbali wa kitaifa, wa sasa na wastaafu.
Amesisitiza kuwa wananchi wote wa mkoa wa Iringa na maeneo mengine nchini wamealikwa kushiriki kwa heshima na utulivu, akiwakumbusha kuwa marehemu Lukuvi alikuwa kiongozi aliyelitumikia Taifa kwa muda mrefu na kulitangaza vyema jimbo lake la nyumbani.
Mkuu huyo wa mkoa amesema Serikali itaendelea kutoa taarifa na mabadiliko ya ratiba endapo yatatokea, huku akihitimisha kwa kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumuenzi marehemu kama alivyokuwa akiheshimiwa enzi za uhai wake.

