NA FAUZIA MUSSA

Wizara ya Afya Zanzibar kupitia Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA), imepiga marufuku usafirishaji wa bidhaa za chakula katika meli moja na bidhaa hatarishi zikiwemo saruji, vilainishi vya magari na kemikali, kwa lengo la kulinda ubora na usalama wa chakula na afya za wananchi.

Akizungumza katika ofisi za ZFDA, Mombasa, Unguja, Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, aliwataka wafanyabiashara, waingizaji, wasafirishaji na wasambazaji wa bidhaa za chakula kuzingatia masharti ya usalama wakati wa usafirishaji na uhifadhi wa bidhaa hizo.

Waziri Mazrui amesema uchanganyaji wa bidhaa za chakula na bidhaa hatarishi unaweza kusababisha uchafuzi kupitia kuvuja kwa kemikali, vumbi jembamba, mabaki ya sumu au harufu kali, hali inayoweza kuathiri ubora wa chakula na kuhatarisha afya za watumiaji.

Ameeleza kuwa bidhaa za chakula zikiwemo mchele, unga wa ngano, sukari, tende na mafuta ya kupikia zinapaswa kusafirishwa na kuhifadhiwa kwa kuzingatia masharti yanayolinda usalama wake.

Aidha, amewataka wafanyabiashara na wasafirishaji kuhakikisha vyombo vya usafiri vinavyotumika kusafirisha chakula vinakuwa safi, vikavu na visivyo na mabaki ya kemikali au uchafu mwingine unaoweza kuathiri ubora wa bidhaa hizo.

Mazrui amesisitiza kuwa usalama wa chakula ni jukumu la kila mdau katika mnyororo wa chakula, kuanzia uzalishaji, uingizaji, usafirishaji na usambazaji hadi bidhaa zinapomfikia mtumiaji wa mwisho.

Amesema Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria, kanuni na miongozo inayohusu usalama wa chakula kwa lengo la kulinda afya za wananchi na kuzuia madhara yanayoweza kusababishwa na ulaji wa chakula kisicho salama.

Aidha, amezitaka taasisi nyingine za udhibiti kushirikiana na ZFDA katika kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa kwa ufanisi.

Kwa upande wao, wafanyabiashara waliohudhuria mkutano huo wameahidi kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa agizo hilo, na kusema kuwa watakua mabalozi kwa wafanyabiashara wenzao ili kuhakikisha kila mmoja anashiriki katika kuweka usalama wa chakula na kumlinda mtumiaji.