Na: Silivia Amandius – Kagera
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera linawashikilia askali 13, wakiwemo askari wa wanyamapori wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), askari wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na askari wa Jeshi la Akiba (Mgambo), kwa tuhuma za mauaji ya watu wanne yaliyotokea katika Kijiji cha Kanyamika, Kata ya Karambi, Tarafa ya Kimwani, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tukio hilo lilitokea Oktoba 17, 2026, majira ya saa kumi jioni katika eneo la Kanyamika, kando ya barabara kuu ya Muleba kuelekea Biharamulo, wakati askari hao walipokuwa doria katika pori la Hifadhi ya Misitu ya Ruiga.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamnda wa POLISI mkoa wa kagera Brasius Chatanda amesema kuwa askari hao walikuwa wakitumia gari la Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili 02 JU 0354, mali ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), likiwa na askari wa wanyamapori na askari wengine waliokuwa kwenye doria hiyo.
Katika tukio hilo, watu waliokuwa wakisafirisha mkaa kwa kutumia pikipiki takribani kumi wanadaiwa kukataa kukamatwa na kujaribu kuwanyang’anya askari silaha. Hali hiyo ilidaiwa kusababisha mapambano na matumizi ya silaha aina ya AK-47, ambapo watu wanne walipoteza maisha.
Waliotajwa kufariki dunia ni Osward Yuster, mwenye umri wa miaka 38, mkazi wa Ngote; Pius Charles, miaka 40, mkazi wa Magata; Charles Michael, miaka 35, mkazi wa Ngote; pamoja na Edgar Elias Lukangula, miaka 44, mkazi wa Butembo, aliyefariki dunia alfajiri ya Oktoba 18, 2026, wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera.
Aidha ameongeza kuwa watuhumiwa wanaoshikiliwa kuwa ni Mituni Haji (26), Faustin William Mboko (25), Kingmar Mewama (40), Fluomena Romani France (28), Erick David Muya (25), Yusuph Idd Kweya (26), Emmanuel Sheki Zabron (25), Yusto David (22), Josiah Msafiri Mahenge (26), Farouk Bashiru Mahamudu (24), Baraka Sadoki Kabulo (28), Regan Bwemelo Nikodem (24), Alanus Beyanga Chowe (35) na Andrew Charles Kwiyega (32), anayetajwa kuwa dereva wa TFS.
Aidha, tukio hilo lilisababisha uharibifu wa gari la Serikali la TFS aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili 02 JU 0354, ambapo kioo cha mbele na vioo vya pembeni kwenye milango viliharibiwa.
Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilipata na kukamata vitu mbalimbali vinavyohusiana na tukio hilo, vikiwemo pikipiki 10, magunia 22 ya mkaa, mapanga matano, kofia ngumu mbili, makoti mawili, silaha tatu aina ya AK-47, maganda matano ya risasi za AK-47 pamoja na gari moja aina ya Toyota Land Cruiser mali ya TFS.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera limesema limewachukua watuhumiwa wote kwa ajili ya uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo na kubaini mazingira ya mauaji hayo.
Aidha, Jeshi la Polisi limeendelea kutoa wito kwa wananchi kutii sheria na kuepuka kujichukulia sheria mkononi wanapokutana na mamlaka zilizopewa dhamana ya kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.
Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea, huku watuhumiwa wakitajwa kushikiliwa kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
