Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma 

Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) imesema kati ya wataalamu 22,269 waliosajiliwa katika ngazi mbalimbali, ni wataalamu 4,449 pekee ambao ni wanachama active baada ya kutimiza vigezo vya kitaalamu na kulipa ada bila kuwa na madeni.Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 19, 2026 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, CPSP Godfred Mbanyi, amesema wataalamu 18,220 ambao hawapo katika kundi la active wanatakiwa kukamilisha ulipaji wa ada zao, huku wale ambao wameonyesha nia ya kulipa wakiendelea kufuatiliwa hadi watakapokamilisha madeni yao.

Aidha, Mbanyi amesema kwa mujibu wa kanuni za bodi, mtaalamu ambaye hajalipa ada kwa kipindi cha miezi 24 anatakiwa kufutwa kwenye rejista ya wanachama, jambo ambalo linaweza kumzuia kufanya kazi za ununuzi na ugavi katika sekta ya umma na binafsi.Amesema kufutwa kwa wataalamu hao kunaweza kuathiri utekelezaji wa miradi ya Serikali na shughuli za sekta binafsi, kwa kuwa wataalamu hao wanahusika katika michakato mbalimbali ya ununuzi, ikiwemo tathmini ya zabuni, utangazaji wa zabuni na majadiliano ya mikataba kupitia mfumo wa NeST.

Pia ameongeza kuwa wataalamu ambao wameanza kulipa madeni yao na kuandika barua za kujikomiti wataendelea kufuatiliwa hadi Desemba 31, 2026, huku bodi ikiendelea kuhuisha orodha ya wanachama kila Ijumaa na kuwahamisha wale wanaokamilisha madeni kutoka kundi la inactive kwenda active.Pia, amebainisha Kuwa wale ambao hawajaonyesha nia yoyote ya kulipa ada zao watafikiwa kupitia waajiri wao, ili kuhakikisha ulipaji unafanyika na kuzuia athari katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali na taasisi binafsi.

Ameongeza kuwa mtaalamu anapokuwa inactive, pamoja na kupoteza baadhi ya haki zake za kitaaluma, hali hiyo pia humzuia mwajiri kupata usaidizi wa bodi katika masuala ya kinidhamu yanayohusiana na taaluma hiyo.Aidha, amesema PSPTB inafikiria kuunganisha mifumo yake na mifumo mingine ya Serikali ili kuwezesha ulipaji wa ada kwa njia rahisi, ikiwemo uwezekano wa makato ya moja kwa moja, baada ya mfumo wa bodi kukamilishwa na kusafishwa taarifa za wataalamu.

Ameongeza kuwa uzingatiaji wa sheria na taratibu katika taaluma ya ununuzi na ugavi umeendelea kuimarika, akisema hatua zinazochukuliwa na bodi pamoja na taarifa za CAG na PPRA zimechangia kuongeza uwajibikaji na weledi miongoni mwa wataalamu.

( Picha zote na Fullshangwe Blog )