Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, amekutana na Balozi wa Shirikisho la Khoja Shia Ithna-Asheri Jamaats ya Afrika, Alhaj Aunali Khalfan pamoja na familia za wanachama walioathirika na mgogoro wa Iran tarehe 26 Machi 2026 katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Balozi Mussa ameeleza shukrani za kipekee kwa wawakilishi hao kwa hatua hiyo ya kufika Wizarani. Aidha, amesisitiza dhamira ya serikali kuendelea kuwasaidia raia wake ndani na nje ya nchi wakati wowote.
Alhaj Khalfan ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuratibu zoezi la kuwarejesha wanafunzi kutoka maeneo ya machafuko nchini Iran.
Naye, Bi. Zia, mzazi wa mmoja wa vijana waliorejea na mwanachama wa Shirikisho la Khoja Shia Ithna-Asheri Jamaats, ameeleza hofu kubwa ya wazazi wakati wa mgogoro huo, na kutoa shukrani kwa Wizara pamoja na Idara yake ya Mashariki ya Kati chini ya Balozi Abdallah Kilima kwa msaada wao endelevu uliowezesha kurejea salama kwa wanafunzi kwa familia zao. Pia aliomba msaada huo wa haraka uendelee kutolewa kwa raia wengine wa Tanzania watakaoweza kukumbwa na majanga ya aina mbalimbali yenye kuhatarisha uhai wao.
Wawakilishi hao wamethibitisha dhamira yao ya kuendelea kushirikiana na taasisi za serikali, wakieleza zoezi hilo kuwa mfano wa diplomasia inayojali watu na yenye mwitikio wa haraka.

