NA DENIS MLOWE – SINGIDA

KATIKA hatua inayoonyesha dhamira ya kuunga mkono maendeleo ya elimu na michezo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Wazohuru Media Group Limited, Mathias Canal, amekabidhi vifaa vya michezo vyenye thamani ya shilingi milioni 4.2 kwa shule kadhaa za msingi katika Manispaa ya Singida.

Msaada huo umetolewa kama sehemu ya maandalizi kuelekea uzinduzi wa WazoHuru Air BnB Apartments zilizojengwa katika Mtaa wa Unyankae–Miembeni, mradi ambao umekamilika kupitia ujenzi wa majengo saba ya makazi ya kisasa yanayotarajiwa kuboresha huduma za malazi mjini Singida.

Shule zilizofikiwa na msaada huo ni pamoja na Tumaini Viziwi, Ukombozi, Kindai, Sumaye, Mtipa na Unyankae. Kila shule ilipokea jezi seti moja yenye jezi 16 pamoja na mpira mmoja wa michezo.

Mbali na shule hizo, Canal pia ametoa vifaa hivyo kwa timu ya Umoja wa Michezo na Taaluma Tanzania kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya mwaka 2026.

Akizungumza wakati wa makabidhiano, Canal alisema kuwa mchango huo ni sehemu ya kuhamasisha michezo mashuleni na kufungua fursa zaidi kwa wanafunzi kuibua na kuendeleza vipaji vyao. Alibainisha pia kuwa kampuni yake imechukua hatua hii kama sehemu ya kurudisha kwa jamii kutokana na mafanikio ya ujenzi wa WazoHuru Apartments.

Uzinduzi rasmi wa mradi huo utafanyika Machi 28, 2026 kuanzia saa 12 jioni, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego.