MDAU katika Sekta ya Nishati ya mafuta nchini Dkt Sajad Habib Rai ameishauri Serikali iangalie jinsi ya kupunguza gharama katika mafuta yanayoingizwa nchini na kusafirishwa kwenda nchi za jirani hatua itakayoliongezea Taifa mapato

Akizungumza Jijini Dar es Salaam Dkt Sajad ambaye pia ni Meneja Mkazi wa Mansoor Industries, amesema kwa kufuata ushauri huo, kutaiwezesha Tanzania kupitia Bandari yake kuongeza idadi ya meli zinazoshusha nishati hiyo sambamba kuongeza mapato kwa wasafirishaji wa Malori wa hapa nchini.

” Kama gharama zitapunguzwa kwa mafuta yanayoingia kupitia Bandari yetu, kimsingi hata idadi ya meli zinazoshusha mafuta zitaongezeka, hii inafanyika kwa Bandari nyingi Barani Afrika, mfano mmoja wapo ni Bandari ya Beira iliyopo nchini Namibia” amesema Dkt Sajad

DKT Sajad pia amesisitiza kuwa kwa kufanya hivyo Tanzania kupitia Bandari yake pia itaongeza fursa kwa watoa huduma za usafirishaji wa mafuta hayo hususani Kampuni za Malori kwa kuwa uingiaji wa kiasi kikubwa cha mafuta kutahitaji huduma zaidi za usafirishaji wake.

Aidha katika hatua nyingine Dkt Sajad ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuilinda bei ya mafuta nchini hatua iliyopelekea bei ya Nishati hiyo kuwa chini zaidi ikilinganishwa na baadhi ya nchi jirani.

Kauli ya Dkt Sajad imekuja siku mbili baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za Nishati na Maji(EWURA) kutangaza bei kikomo za Mafuta kuanzia Juni 3, 2026 zitakazotumiwa na wafanyabiashara wote wa nishati hiyo maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa EWURA,bei hizo mpya zinaonyesha kuwa Petroli katika Dar es Salaam itauzwa kwa Sh. 4,086 kwa lita, Dizeli Sh. 4,333 na mafuta ya taa Sh. 4,685 kwa lita, jambo ambalo Dkt Sajad anasema linatoa matumaini kwa wananchi.

Akizungumza zaidi kuhusu hatua hiyo Dkt Sajad amesisitiza hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kuhakikisha bei ya mafuta haileti makali kwa wananchi licha ya mgogoro ambao bado unaendelea katika Mataifa ya Mashariki ya kati.

“Tunaipongeza Serikali kwa kuendelea kuhakikisha bei ya mafuta nchini inaleta unafuu kwa wananchi, hii inaonesha ni kwa kiasi gani inawajali wananchi wake, hii ni hatua nzuri ambayo baadhi ya nchi wameshindwa kufanya hivyo” amesema Dkt Sajad

Amesema uwepo wa mgogoro katika Mataifa hayo uliopelekea pia kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz na hivyo kusababisha kuongezeka kwa gharama za mafuta katika soko la dunia, ni jambo lililosababisha pia kupanda kwa gharama za bidhaa mbalimbali mbali na mafuta.

Kulingana na tangazo lililotolewa na Ewura, bei ya Petroli imepungua kwa zaidi ya Sh. 30 kwa lita ikilinganishwa na mwezi uliopita huku Dizeli ikiendelea kubebwa na ruzuku ya Shilingi 534.91 kwa kila lita, sawa na Shilingi 535.

Kimsingi kipindi hiki ambacho mataifa mengi Duniani yanakabiliwa na kupanda kwa gharama za nishati na changamoto za upatikanaji wa mafuta, Tanzania imeendelea kuwa na bei nafuu zaidi ya petroli na dizeli miongoni mwa nchi zilizolinganishwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini ikichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuweka ruzuku ya Sh. 535 kwa kila lita ya dizeli.

Hatua hiyo pamoja na mambo mengine kwa kiasi kikubwa imeendelea kuisaidia sekta za usafirishaji, viwanda, kilimo na huduma za kijamii ambazo zinategemea zaidi mafuta hayo.