Kaimu Waziri wa Utalii na mambo ya Kale Mudrik Ramadhan Soraga akizungumza na Waandishi wa Hbari kuhusiana na Mafanikio na Maendeleo ya Wizara kutimia Siku Mia Moja za Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Barza la Mapinduzi Dk,Hussein Ali Mwinyi kwa kipindi Chake cha Pili hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo Rahaleo Zanzibar.

………….

Na Maelezo Zanzibar 24.03.2026

Serikali inaendelea kuimarisha usimamizi wa Mji Mkongwe kwa kuzingatia sheria na mikataba ya kimataifa ya UNESCO ambapo maeneo 85 ya kihistoria yametambuliwa rasmi na hatua zinaendelea kuipa hadhi ya kisheria.

Akizungumza katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar wakati akizungumza na waandishi wa habari katika siku 100 za Mafanikio za Uongozi wa Dk. Mwinyi, Kaimu Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga amesema serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi pamoja na washirika wa maendeleo katika uwekezaji na uhifadhi wa urithi wa kihistoria, jambo linachangia ukuaji wa uchumi wa nchi.

Aidha Waziri Soraga amesema kuwa Serikali inaendelea na ukarabati wa majengo muhimu ya kihistoria ikiwemo jengp la Beit el Ajaib, Kasri la Maruhubi, Kasri la Mtoni pamoja na maeneo ya kihistoria Unguja na Pemba, miradi hiyo inalenga kuhifadhi historia, kuvutia watalii na kuongeza mapato ya Taifa.

Akizungumzia Sekta ya Utalii, amesema Serikali inaendelea kuweka mikakati thabiti ya kukuza sekta hiyo kwa kuzingatia utalii endelevu, ubora wa huduma, na ushirikishwaji wa wananchi.

“Sekta hii imechangia kwa kiasi kikubwa katika pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 30%, ajira zaidi ya 65,000, mapato ya Serikali na ustawi wa wananchi” ameeleza.

Amefahamisha kuwa katika kipindi hichi idadi ya watalii imeongezeka na kufikia watalii 273,773 kutoka mataifa mbalimbali ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 115 sawa na kipindi cha mwaka 2020/2021 sambamba na muda wa ukaazi wa wageni umeongezeka kutoka siku 6 hadi siku 8, jambo linaloongeza mapato ya faida kwa wananchi.

“Kwa upande wa uwekezaji, tumeshuhudia ongezeko la vyumba vya hadhi ya juu hadi kufikia zaidi ya 17,000, hatua inayolenga kuvutia watalii wenye matumizi makubwa Sambamba na hilo, Wizara inaendelea kuelimisha wadau wa sekta, kurasimisha huduma za (beach boys na beach girls), na kuimarisha usimamizi wa Bahari kwa kushirikiana na Wizara ya Uchumi wa Buluu kupitia mpango wa (Marine Spatial Planning)”, amesema Mhe. Soraga.

Aidha amesema kuwa katika kuendeleza utalii wa kijamii na wa vijijini (Community based) Serikali inaendelea kuibua na kuimarisha vivutio vipya, hususan katika Kisiwa cha Pemba pamoja na kushirikiana na wadau mbali mbali ili kuendelea na hatua za kukamilisha Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Utalii Pemba ili kukifungua Kisiwa hicho kwa uwekezaji na kukuza Sekta ya Utalii inayozingatia matakwa ya wananchi ikiwemo mazingira endelevu.

“Miradi ya vivutio vya utalii wa kijamii kama vile Pango Samaki, Kisiwa Ndege, Pemba Fox na vijiji vya utamaduni inaendelea kutekelezwa” alibainisha Waziri Soraga.