Na John Walter-Simanjiro

Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Simanjiro wameadhimisha Wiki ya Maji kwa kuendesha zoezi la upandaji miti katika vyanzo vya maji mbalimbali wilayani humo, ambapo jumla ya miti zaidi ya 1,534 inatarajiwa kupandwa.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Machi 19, 2026 katika Kitongoji cha Lengungumwa, Kijiji cha Nyumba ya Mungu, Kaimu Meneja wa RUWASA Simanjiro, Mhandisi Wilson Mollel, alisema katika kitongoji hicho tayari miche 100 ya miti imepandwa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za wilaya nzima kulinda vyanzo vya maji na kuhifadhi mazingira kwa ujumla. 

Aliongeza kuwa zoezi hilo linaendana na kaulimbiu ya Wiki ya Maji isemayo “Maji na Jinsia.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chombo cha Watoa Huduma ya Maji ngazi ya Jamii (CBWSO), Ndg. Patrick Mbogo, akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji wa Lengungumwa, alisema mradi umekamilika na unahudumia wananchi wapatao 736 kutoka kitongoji hicho pamoja na vijiji jirani.

 Aliongeza kuwa mradi huo umewezesha ukusanyaji wa mapato yaliyofikia shilingi milioni 14.6 ndani ya kipindi cha miezi sita.

“Mradi huu umechangia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji, kutoa ajira kwa wakazi wa eneo husika, na kuongeza mapato yanayosaidia uendeshaji wake bila kutegemea ruzuku ya serikali.

Aidha, umewezesha pia upatikanaji wa maji kwa mifugo, tofauti na hapo awali ambapo ililazimika kuswagwa umbali mrefu kwenda kunywa maji mtoni,” alisema Ndg. Mbogo.

Naye Mtendaji wa Kata ya Ngorika, Bi. Getrude Shauri, ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa maji kupitia mradi huo.

Alibainisha kuwa kabla ya mradi huo, wananchi, hususan wanawake, walilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

Bi. Shauri aliwahimiza wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya maji na mazingira ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji, pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Ni wajibu wa kila mmoja kulinda rasilimali hizi muhimu kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo,” alisisitiza.