Na Mwandishi Wetu, Rukwa–Kalambo

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Kalambo kwa kushirikiana na taasisi binafsi ya Roots and Shoots, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na wadau wa mazingira, wamepanda miche 1,300 ya matunda na miti ya mbao katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kalambo, sambamba na kutoa elimu ya uhifadhi kwa wanafunzi.

Zoezi hilo lililofanyika Machi 21, 2026 ikiwa ni kilele cha Siku ya Misitu Duniani, lilihusisha upandaji wa miti ya vivuli, matunda na mbao pamoja na utoaji wa elimu ya vitendo kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira.

Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mheshimiwa Peter Lijualikali ambaye anakaimu Wilaya ya Kalambo, alizindua kampeni hiyo ya upandaji miti kiwilaya na kutoa wito kwa makundi yote kutumia mvua zinazoendelea kunyesha kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Pia aliagiza TFS kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waharibifu wa mazingira wanaokata miti ovyo na kuchunga mifugo hifadhini, akisisitiza umuhimu wa wanafunzi kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira.

Aidha, Mhifadhi Misitu wa Wilaya ya Kalambo, Mhifadhi Mwandamizi (SCO) Braison Mkiwa alisema kuwa hadi sasa miti 317,500 ya aina mbalimbali imepandwa wilayani humo kuanzia Desemba 2025 hadi Machi 2026, huku zoezi hilo likiendelea kwa ushirikiano wa taasisi, vikundi, shule na watu binafsi.

Kwa upande wake, mdau wa mazingira kutoka Taasisi ya Jane Goodall Institute kupitia Roots and Shoots alisema kampeni hiyo inalenga kubadili mtazamo wa jamii, hususan wanafunzi, ili kutambua kuwa uhifadhi endelevu ni msingi wa uchumi endelevu.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kalambo alisema upandaji miti na uhifadhi wa mazingira ni muhimu kwa kizazi cha sasa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.