NA DENIS MLOWE, IRINGA

WANANCHI wa mtaa wa Kitasengwa ulioko katika kata ya Isakalilo manispaa ya Iringa wamesema kuwa wanaishi kwa hofu na uchungu kutokana na hali mbaya ya miundombinu, hususan barabara ambazo zimeharibika vibaya baada ya mvua kubwa kunyesha.

Wakazi hao wanasema kuwa licha ya changamoto hiyo kuanza tangu mwaka jana, bado hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa na viongozi wa ngazi mbalimbali.

David Nyinge, mkazi wa eneo hilo, amesema kuwa wananchi wameachwa wakiteseka bila msaada wowote, huku barabara zilizochanwa tangu kipindi cha uongozi wa aliyekuwa meya Kimbe zikibaki katika hali mbaya.

Ameeleza kuwa hakuna ufuatiliaji wa miundombinu na wananchi wamelazimika kuchukua hatua za kuchangishana ili kufanya marekebisho madogo kwa kununua kalavati walizojipangia wenyewe.

Amefafanua kuwa licha ya kuwasilisha malalamiko kwa madiwani na watendaji wa eneo hilo, hakuna msaada walioupata. Ameongeza kuwa baadhi ya maeneo bado hayapitiki, na wananchi wamelazimika kujitolea kurahisisha mawasiliano kwa kadiri ya uwezo wao.

Kwa upande wake, Cecilia Stefano Ugi, ambaye ni balozi wa mtaa wa Shina namba tano, amesema kuwa barabara ya Mikwere imekatika vibaya kiasi cha kuathiri shughuli za kila siku amesema kuwa akina mama wajawazito na wagonjwa wako hatarini kwani ni vigumu kuwafikisha hospitali zilizopo maeneo ya Flerimo au hospitali ya rufaa ya mkoa.

Amesema kuwa juhudi za awali za kuweka maroba mwaka jana zilisaidia kwa muda mfupi, lakini mvua za mwaka huu zimeharibu zaidi barabara hiyo.

Ameomba uongozi wa ngazi ya kata na ngazi za juu kuchukua hatua haraka kwa kuweka makaravati ili kuruhusu maji kupita na kuokoa maisha ya wananchi.

Theresia Haule, mkazi mwingine wa eneo hilo, amesema mvua za jana zimezidisha uharibifu, na watoto wanaokwenda shule wanashindwa kuvuka eneo lenye Korongo.

Amesisitiza kuwa wananchi wanateseka na wanahofia makazi ya watu wanaoishi maeneo ya chini ambayo yanakumbwa na mafuriko kila mvua inaponyesha.

Amesema kuwa familia nyingi ziko katika hatari endapo mvua zitaendelea, na ameomba viongozi wakuu kusikiliza kilio cha wakazi wa Kitasengwa na kuchukua hatua za haraka ili kuzuia madhara zaidi.

Wananchi wameendelea kutoa wito kwa serikali na wadau mbalimbali kuchukua hatua za dharura kushughulikia tatizo hilo ambalo limekuwa likiendelea kwa muda mrefu na sasa limefikia hatua ya kuhatarisha maisha na usalama wa wakazi wa eneo hilo.

Akizungumza kwa niaba ya mwenyekiti wa mtaa, mjumbe wa serikali ya mtaa huo, Wazarudi Masika, ameeleza kuwa Mwenyekiti yupo kwenye majukumu mengine ya dharura yanayohusiana na maafa, na hivyo akamtuma kufika katika eneo hilo ili kushirikiana na wananchi kutafuta suluhisho la haraka.

Masika amesema kuwa wananchi walimweleza kuwa wapo katika njia panda na wanahitaji hatua za dharura za kupunguza athari za mafuriko na baadhi ya wananchi walipendekeza kuendelea kuweka mawe katika maeneo yaliyokatika ili kupunguza kasi ya maji, ingawa jitihada hizo za awali zilishindikana kutokana na maji kugonga na kubomoa ukuta uliokuwepo.

Wananchi waliona umuhimu wa kuchukua hatua za muda mfupi kabla ya kufikiria hatua rasmi za ngazi za juu, kwani nyumba zilizo karibu na mtiririko wa maji, ikiwemo nyumba ya mama mmoja mkazi wa eneo hilo, ziko katika hatari kubwa endapo mvua zitaendelea kunyesha.

Masika ameeleza kuwa wananchi walipendekeza kutafuta maroba kwa ajili ya kuziba maeneo hatarishi kama hatua ya muda, huku wakisubiri taratibu rasmi za serikali kuendelea.

Aidha, alisema kuwa wananchi waliona umuhimu wa kupata mtaalamu wa kufuatilia hali hiyo kitaalamu mmoja wa wananchi ambaye pia ni fundi ujenzi alitoa maoni kuwa suluhisho la kudumu ni kuweka kalavati.

Baada ya majadiliano hayo, Masika alimpigia mtendaji wa mtaa ambaye alikuwa katika safari ya kwenye msiba wa ndugu wa mtumishi mwingine wa eneo hilo hata hivyo, mtendaji aliahidi kuwa kesho atakuwepo kushirikiana na wananchi katika kutafuta ufumbuzi.

Masika amebainisha kuwa mchakato wa kupata kalavati unahitaji kufuata taratibu za kiutawala kuanzia kwa mwenyekiti wa mtaa, mtendaji wa mtaa, mtendaji wa kata, kisha hatua za juu zaidi.

Alisisitiza kuwa kalavati zinaweza kupatikana lakini ni lazima wananchi waendelee kufuata utaratibu huo hata hivyo, kwa dharura iliyopo, wananchi wamekubaliana kuchukua hatua za muda za kuzuia maji kwa siku chache zijazo huku mchakato rasmi ukiendelea.

Ameongeza kuwa endapo hatua hizo zitafanikiwa, maeneo yanayokumbwa na mafuriko yatapunguziwa athari kwa kiasi kikubwa, na wananchi wataweza kurudi katika shughuli zao za kila siku.

Wananchi wa Kitasengwa wanaendelea kuomba serikali na wadau mbalimbali kuingilia kati kwa haraka ili kuokoa maisha, makazi na miundombinu ambayo ni muhimu kwa ustawi wa jamii hiyo.